Makonda akataza bomoabomoa haramu Dar


Salha Mohamed

Paul Makonda
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewaagiza wakuu wa wilaya mkoani mwake, kutokubali kubomolea nyumba wananchi bila kujiridhisha kwa hukumu halali za Mahakama.

Pia Jeshi la Polisi limetakiwa kutosimamia mchakato wa ubomoaji nyumba bila Mkuu wa Wilaya kujiridhisha na uhalali wa kubomoa.

Makonda alisema hayo jana wakati akimwapisha Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori aliyechukua nafasi ya Humphrey Polepole aliyeteuliwa kuwa Katibu Mwenezi wa CCM.

Alisema kuna tabia mkoani humo ya watu kutekeleza hukumu za Mahakama na zingine zikiwa feki kwa kubomolea wananchi nyumba zao.

“Hakuna mtu anayeruhusiwa kubomoa nyumba bila ninyi (wakuu) kujiridhisha kwamba ana hukumu halali ya Mahakama, kama hana hukumu halali una nafasi ya kuchukua hatua,” alisema huku akibainisha kutumia wanasheria wa mkoa na manispaa hizo kupitia nyaraka zote.

”Kwa hiyo wale wote sijui Majembe Auction … hawaruhusiwi kubomoa nyumba hadi DC uwe na uhakika kwamba hatua za hukumu zimepitishwa kihalali,” alisema.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia kuzuia kilio cha wanyonge na masikini ambao wanabomolewa nyumba na baada ya siku inagundulika kuwa hukumu ni bandia.

“Nawaagiza wakuu wa wilaya simamieni hilo, ili mwakani tuongeze kasi ya kutetea wanyonge. Hakuna mtu mwenye mamlaka ya kubomoa nyumba kama wewe hujaridhika,” alisema.

Makonda aliitaka Polisi kutoshiriki mchakato wa kuvunja nyumba za wananchi hadi DC atakapojiridhisha.  

Makori, alisema anatambua wilaya hiyo ina changamoto nyingi za huduma za maendeleo wanayohitaji.

“Viongozi nitakaokuwa nao katika majukumu haya, tushirikiane kuhakikisha tunatatua kero na matatizo ya nchi, kwani siasa nzuri ni ya kuleta maendeleo na kubadilisha maisha ya watu yawe tofauti na yalivyo sasa,” alisema.

Aliwahakikishia wananchi kuwa na nia ya kufanya kazi na si porojo na kufanya mambo yatakayoleta ahueni kadri fursa itakapojitokeza kwa wananchi wa Ubungo kuona tofauti.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo