Achomwa mkuki mdomoni, atembea nao kwa saa saba


Peter Kimath, Morogoro

MKAZI wa Kijiji cha Dodoma Isanga Kata ya Masanze wilayani Kilosa, Agustino Mtitu amepigwa mkuki mdomoni na kutokea upande wa pili wa shingo na wafugaji akiwa katika harakati za kuzuia mifugo iliyoingia shambani na kula mazao.

Diwani wa Kata ya Msanze, Bakari Kilo alisema kuwa Desemba 25 mwaka huu, majira ya saa 3:00 asubuhi alipigiwa simu na wananchi akielezwa kuwa kuna mifugo imeingia katika Kijiji cha Dodoma Isanga na kuharibu mazao shambani.

Bakari alisema wakulima wakiwa wanazuia ngo’mbe kula mazao, ndipo lilipotokea kundi la wafugaji na kuanza kulumbana na wakulima hao.

Wakiwa kwenye majibazano, mfugaji mmoja alimpiga Agustino Mtitu mkuki wa mdomoni.

Alisema Mtitu alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa matibabu, lakini walishindwa kumtibu jeraha hilo na alisafirishwa kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.

Alisema wakiwa katika harakati za kushughulikia mgonjwa huyo, wakulima walizuia mifugo ya wafugaji ili ajitokeze mwenye mali lakini walishindwa kufutia kundi la wafugaji kufika eneo na kuanza kuwashambulia.

Aliwataja walioshambuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya Kilosa ni Yohana Wise, Josephati Mtitu, Paulo Thomas, Mathayo Elias na George Andrea, hali zao zinaendelea vizuri.

Bakari aliwataka wafugaji kuheshimu maeneo ya wakulima na kwenda kwenye maeneo yao, huku akiomba jeshi la polisi kuwachukulia hatua waliofanya vurugu hizo.

Kwa upande, Daktari wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk Frank Jakobo alisema Desemba 25 majira ya saa 10 jioni, walipokea mgonjwa aliyetambulika kwa jina la Agustino Mtitu kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kilosa akiwa na mkuki mdomoni.

Dk Frank alisema hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri na walifanikiwa kumtoa mkuki huo mdomoni tangu juzi na sasa anaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari.

Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mikumi kupitia katibu wake, Robert Galamona imelaani kitendo kilichofanywa na wafugaji hao na kuiomba Serikali kuwabaini waliofanya kitendo hicho cha kinyama.

Galamona alitaka wahusika wapewe adhabu kali kwa mujibu wa sheria na ili iwe fundisho kwa wananchi wenye tabia ya kujichulia sheria mkononi pindi inapotokea kutofautiana kati ya pande mbili.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alithibitisha tukio hilo na kusema bado jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini wahusika na kuwafikisha mbele ya sheria.

Wilaya ya Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro zimekuwa  vinara kwa vurugu za wakulima na wafugaji kwa miaka mingi na hadi sasa hakujawa na suluhu ya kudumu iliyopatikana kuhusu migogoro hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo