Tume yataka sheria, kanuni zizingatiwe kazini


Abraham Ntambara

Jaji Steven Bwana
TUME ya Utumishi wa Umma nchini imezitaka mamlaka za ajira, watumishi wa umma na waajiri kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na nidhamu wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Steven Bwana ilisema Tume ilifanya mkutano wa wiki mbili ikapokea na kujadili taarifa za ukaguzi wa rasilimaliwatu katika taasisi kadhaa za umma.

Alisema miongoni mwa taasisi zilizojadiliwa ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Uendelezaji Makao Makuu Dodoma (CDA), wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA), Manispaa ya Ilala na Manispaa ya Kinondoni na kubaini ukiukwaji wa taratibu.

“Katika kaguzi hizo na kushughulikia rufaa ilibainika kuwepo kwa ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu miongoni mwa watumishi wa umma, waajiri, mamlaka za ajira na nidhamu,” alisema Jaji Bwana.

Alisema baadhi ya viashiria vikubwa vya udhaifu vilivyojitokeza ni pamoja na tabia mbaya kwa baadhi ya watumishi wa umma iliyosababisha kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria na kinidhamu.

Viashiria vingine alisema ni mamlaka za nidhamu kushindwa kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria watumishi wenye utendaji mbovu, huku baadhi ya mamlaka zikishindwa kuunda kamati za uchunguzi au kutotumia taarifa za uchunguzi wa awali kama zilivyowasilishwa kwao.

Aliongeza kuwa vingine ni kufungua mashauri ya nidhamu na kukaa muda mrefu bila kuyahitimisha huku pia wakibaini upungufu kwenye uandaaji na uendeshaji mchakato wa mashauri.

Jaji Bwana alisema walibaini upandishwaji vyeo watumishi bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ambapo Tume ilisisitiza watumishi wa umma, waajiri na mamlaka za nidhamu kuzielewa na kuzizingatia wakati wote.

Aliwataka viongozi wa halmashauri waelewe, wazingatie na waelimishe watendaji wa vijiji na kata kuhusu umuhimu na uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu wakati wanapotekeleza majukumu yao.

Alisema kwenye mkutano huo wa wiki mbili Tume ilishughulikia na kutoa uamuzi wa rufaa 42 na malalamiko mawili ambapo rufaa 31 zilikataliwa na nane kukubaliwa bila masharti huku tatu zikikubaliwa kwa masharti kwa kutakiwa kuanza upya kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo