Wanahabari wakerwa na Mkuu wa Wilaya


Waandishi Wetu, Arusha

William Lukuvi
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ameshuhudia Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti akizomewa na waandishi wa habari baada ya kugoma kuzungumzia hatima ya mwandishi wa kituo cha ITV, Halfan Lihundi aliyewekwa mahabusu kwa amri yake.

Waandishi wa habari jana walikusanyika kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Arusha kusubiri kuzungumza na Waziri huyo kuhusu hatima ya Lihundi na alipotoka kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa akifuatana na Mkuu huyo wa Wilaya, walimtaka Mkuu wa Wilaya azungumze lakini aligoma na kukimbilia kwenye gari lake ndipo wakamzomea.

Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema uandishi wa habari ni taaluma na ina Waziri husika, hivyo asingeweza kuzungumzia sakata la kukamatwa kwa Lihundi na badala yake watafutwe viongozi wahusika wa tasnia ya habari.

Akiwa anazomewa na wanahabari hao, Mnyeti alisikika akilalamikia waandishi kumfuata kwani alishatoa maagizo ya kuachwa kwa Lihundi.

"Ole wake mtu anifuate, hata hivyo nimeshasema wamwache kwa nini wananifuata hadi huku?” Alisikika Mkuu huyo akihoji huku akielekea kwenye gari lake akirusha mikono.

Jana asubuhi kabla ya kwenda ofisi za Mkuu wa Mkoa kuonana na Lukuvi, waandishi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Arusha, Claud Gwandu waliazimia kutoripoti habari za Waziri Lukuvi ambaye anatembelea wilaya ya Arumeru na endapo atatokea mwandishi akakiuka makubaliano hayo atatengwa.

Polisi  

Jana waandishi  walikusanyika nje ya kituo cha Polisi cha Usa River wakati Lihundi akiendelea kushikiliwa kwenye mahabusu ya kituo hicho cha wilaya.

Akifuatana na wakili wake, Edward Silayo, Lihundi alitolewa nje kwa mazungumzo lakini Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya, alimchukua na kuamuru arudishwe mahabusu kwa alichodai kuwa kukamatwa kwake ni amri ya Mkuu wa Wilaya.

Wakili Silayo aliposema yeye ana uhalali wa kuzungumza na mteja wake, alijibiwa kuwa hakuna kesi iliyofunguliwa kituoni hapo na kilichofanyika ni Lihundi kuwekwa mahabusu kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ambaye kisheria anaruhusiwa kumshikilia mtu yoyote kwa saa 48.

Hata hivyo, ilipofika saa 7 mchana mmoja wa wapelelezi wa Polisi alimtaka wakili Silayo aingie kwenye chumba cha mahojiano ili Lihundi ahojiwe na kuachwa.

Wakati mahojiano hayo yakiendelea, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Arumeru, alifika na kumtaka ofisa wa Polisi aliyekuwa akimhoji Lihundi kuacha mahojiano na kuingia na Lihundi na Wakili Silayo kwenye chumba kingine.

Wakiwa kwenye chumba hicho, Lihundi alihojiwa upya chini ya Silayo na walipomaliza, aliachwa kwa dhamana.

Wadau mbalimbali wa habari nchini walikosoa kukamatwa kwa mwandishi huyo kwa tuhuma za kuandika habari za kichochezi.

Ilidaiwa jana na wadau hao kuwa hatua hiyo ilichukuliwa na Mkuu wa Wilaya kutokana na uoga wa kutojua namna  bora ya kutekeleza  majukumu yake kwa wananchi.

Mmoja wa wadau hao ni mwandishi mkongwe wa habari, Joseph Sabinus aliyesema kuwa kiongozi mchapakazi na mwelewa wa majukumu yake hawezi kuogopa kukosolewa na kutaka kupongezwa tu.

“Kupongezwa ni dalili za kufungwa macho, hivyo ni bora ukosolewe ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo,” alisema.

Alishauri viongozi wasiogope kukosolewa, kwani jukumu la mwandishi wa habari na chombo cha habari, ni kufichua na kuibua kero za wananchi na si kusifu viongozi.

Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena alisema mwandishi wa habari ana wajibu wa kuandika kero za wananchi  na kuzungumza na Mwenyekiti wa Kijii, Mtendaji, Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa.

Alisema viongozi hao wanaweza kufanikisha habari hiyo kuwa sahihi kwa kuzungumza na mamlaka husika kuhusu kero zinazokabili wananchi katika eneo husika.

“Hatuwezi kuvumilia vitendo vya unyanyasaji waandishi ukiendelea, lazima hatua zichukuliwe kwa kuzingatia taaluma na kilichoripotiwa kilikuwa ni kwa faida ya nani,” alisema.

Mkurugenzi wa Habari-MAELEZO, Dk Hassan Abbas alisema Serikali inafuatilia kupata uhakika wa tukio hilo na baadaye kulitolea ufafanuzi.

“Bado tunaendelea kufuatilia ili kupata maelezo kamili baada ya tukio hilo,” alisema.

Juzi Lihundi alikamatwa na polisi wa Usa River kwa tuhuma za kuandika habari zinazodaiwa kuwa za uchochezi.

Lihundi alikamatwa saa nane mchana na askari aliyepewa agizo na Mnyeti kwa madai ya kuandika habari ya uchochezi kuhusu malalamiko ya wananchi wanaokabiliwa na tatizo la maji.

Gwandu alilaani kitendo hicho na kusema hatua hiyo haikubaliki kwani haikufuata taratibu.

MCT

Sijawa Omary kutoka Mtwara anaripoti kuwa Baraza la Habari Tanzania (MCT) limetoa tamko la kulaani na kutoridhishwa na kitendo cha kukamatwa kwa Lihundi.

Tamko hilo lilitolewa jana mkoani humo na Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga  alipozumgumza na waandishi wa habari wa mkoa huo aliko kwa majukumu ya kikazi.

Habari iliyoripotiwa ilihusu mgogoro wa maji katika kijiji cha Leguruki juu ya wananchi wa kijiji hicho kukosa maji kwa siku kadhaa.

Mukajanga alisema mwandishi wa habari ana haki ya kupata habari na kuitoa kwa maslahi ya umma bila kuvunja sheria ikiwa ni moja au sehemu ya majukumu yake.

“Suala la kumfanya mwandishi wa habari ashindwe kutimiza majukumu yake kikatiba ni kinyima uhuru wa vyombo vya habari pia ni kumfanya mwananchi ashindwe kupata habari kama haki yake ya msingi na kikatiba,” alisema Mukajanga.

Alisema Serikali inataka utendaji wa uwajibikaji, kufichua na kupambana na vitendo viovu ikiwamo rushwa lakini inashangaza kuona mwandishi akitekeleza sehemu ya majukumu yake anakuwa mchochezi hivyo kumnyima uhuru wa kufanya kazi yake kikamilifu.

Mwenyekiti  wa Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Mtwara (MTPC), Hassan Simba alisema wanahabari wa mkoa wanalaani  kitendo cha kukamatwa kwa mwandishi huyo, kwani ni udhalilishaji dhidi ya waandishi wa habari nchini na duniani kote.

Imeandikwa na Seif Mangwangi (Arusha), Sijawa Omary (Mtwara), Leonce Zimbandu na Sharifa Marira (Dar es Salaam).
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo