RC awapoza waathirika wa tetemeko


Peter Akaro

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu, Salum Kijuu jana alitumia hadhara ya Ibada ya Krismasi kuwapoza waathirika wa tetemeko la ardhi lililoukumba mkoa huo hivi karibuni, akisema misaada yote inayotolewa inasimamiwa na Serikali.

Akizungumza katika Ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika kitaifa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Magharibi Bukoba, Kijuu mbali na kuwapongeza waliotoa misaada hiyo, alisema hakuna msaada utakaotumika kinyume kwa kuwa inasimamiwa na kamati ya maafa ya mkoa ambayo yeye ndiye mwenyekiti.

“Serikali inaendelea kutoa shukrani kwa mashirika, taasisi, kampuni na wahisani wote kwa namna walivyoguswa na kujitokeza kuchangia,” alisema Kijuu.

Alisema tetemeko hilo lililoua watu 17 na kuacha majeruhi 440, lilisababisha uharibifu mkubwa wa mali, miundombinu na kuacha simamzi kubwa mioyoni mwa watu wengi.

“Nawashukuru viongozi wetu wa dini zote kwa jinsi walivyoshirikiana na serikali kwa kuwafariji waadhirika waliopatwa na maafa haya,” alisema Kijuu.

Katika hatua nyingine aliwashukuru viongozi wote wa dini mkoani Kagera na madhehebu yote kwa ushirikiano pamoja na serikali kwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kikamilifu na kuwaunganisha wananchi kuwa kitu kimoja.

“Mmeweza kudumisha amani, upendo, utulivu pamoja na kuvumiliana pale linapotokea jambo ambalo linataka kutugawanya katika Imani zetu,” alisema

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Moses Matonya, alisema Jumuiya hiyo imeitika wito wa Serikali wa kuwasaidia kwa hali na mali watu walioathirika na tetemeko hilo.

“CCT kupitia shirika lake imetoa mchango na kuuwasilisha kwa Mkoa wa Mkoa kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo