Wananchi: Ubora wa elimu waongezeka


Abraham Ntambara

TAASISI ya Utafiti ya Twaweza imesema wananchi wanasema ubora wa elimu umeongezeka tangu kuanzishwa kwa mfumo wa elimu bure, huku Watanzania sita kati ya 10 wakisema wangepeleka watoto wao shule binafsi kama wangekuwa na uwezo.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Hali Halisi kuhusu maoni ya wananchi juu ya elimu bure bila malipo.

"Kutokana na kuanzishwa kwa mfumo wa elimu bila malipo, asilimia 50 ya wananchi wanasema ubora wa elimu umeongezeka, lakini asilimia 35 wanasema ubora wa elimu uko palepale huku asilimia 15 wakisema umeshuka," alisema Eyakuze.

Eyakuze alisema muhtasari huo unatokana na takwimu kutoka Utafiti wa Sauti za Wananchi, ambapo matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,806 kutoka maeneo ya Tanzania Bars kati ya Agosti 7 na 14.

Alisema wananchi wengi wana mitazamo chanya juu ya elimu nchini, lakini ni dhahiri kuwa shule za Serikali bado zinakabiliwa na changamoto ambapo kwa mujibu wa wahojiwa, changamoto kuu ni ukosefu wa walimu, madawati, madarasa na uhaba wa vitabu.

Mkurugenzi alieleza, kwamba kwenye kaya nane kati ya 10 zenye watoto, asilimia 90 yao husoma shule za Serikali, hata hivyo alisema iwapo shule za Serikali na binafsi zingekuwa bure, wananchi sita kati ya 10 wanasema wangewapeleka watoto wao shule binafsi.

Alisema hiyo ni ishara kwamba wananchi wana shaka na ubora wa elimu kwenye shule za Serikali ambapo asilimia 45 yao walitaja elimu bora, uwepo wa walimu wanaofanya kazi kwa bidii na wanaopewa motisha ni asilimia 12, pamoja na idadi ya kutosha ya walimu ni asilimia 12, hizo zilitajwa kama sababu kuu za kuzipendelea shule binafsi.

Alisema wananchi wengi ambao ni asilimia 51 walisema elimu ni bora katika shule za binafsi za msingi na za sekondari ni asilimia 56 ambapo inatofautiana kwa kiasi kikubwa na waliosema shule za Serikali huku  shule za msingi ikiwa ni asilimia 22 na sekondari asilimia 19.

Aidha, alifanua kuwa asilimia 85 ya wananchi walisema kutojihusisha kwa wazazi kwenye masuala ya shule ni changamoto kuu kwenye elimu na kuongeza kuwa changamoto zingine zilikuwa ni pamoja na miundombinu ya shule sawa na asilimia 83, matokeo mabaya ya wanafunzi asilimia 83, nidhamu ya wanafunzi asilimia 79, kutowapa motisha walimu asilimia 66 na ubora wa mtaala asilimia 62.

Alieleza kuwa wazazi kutojihusisha kwenye masuala ya shule kunaashiria katika idadi ya wazazi ambao hawajawahi kutoa msaada wowote kwenye shule za watoto wao na ni sawa na asilimia 88, pia wazazi waliokutana na walimu wa watoto wao, mara moja au mbili kwa mwaka ni asilimia 52.

Aidha, alisema wazazi waliotembelea shule wanazosoma watoto wao mara moja au mbili ni asilimia 57 mwaka uliopita.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo