Wapinzani walia na mambo manne


Abraham Ntambara

VYAMA vya upinzani nchini vimetaja mambo makubwa manne ambayo havitayasahau mwaka huu unaoelekea mwisho wakisema yalikuwa kikwazo na mwiba kwa upande wao.

Wapinzani hao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walimtaja Rais John Magufuli kuwa mhusika wa wao kukumbwa na hali hiyo kwa kuidhinisha mambo hayo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na JAMBO LEO viongozi wa Chadema, NCCR- Mageuzi na NLD, walitaja kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara, maandamano na kutishwa na kuwekwa ndani kuwa viliwabana kisiasa licha ya kuwa ni haki yao kikatiba.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alisema jambo ambalo hawatalisahau na lililowashitua ni kauli ya Rais Magufuli kupiga marufuku shughuli za kisiasa za kufanya mikutano ya hadhara na maandamano.

“Sasa ni sawa na mpishi, unamwambia ni marufuku kupika wakati hiyo ndiyo haki yake, sisi siasa ndiyo kazi yetu, anazuia kazi ambazo ziko chini yetu kihalali,” alisema Mwalimu.

Alisisitiza kuwa suala hilo liliwashitua, ni suala ambalo watalikumbuka na kuongeza kuwa suala lingine lilikuwa ni alichokiita ubabe wa watawala na vyombo vya Dola dhidi ya viongozi wa Chadema ambao walitishwa na hata kupelekwa mahabusu na mahakamani.

Katibu Mkuu wa NLD, Tozi Matwange alisema jambo wasilolisahau ni Rais kuvunja Katiba ambayo aliapa kuitumikia na kuilinda ikiruhusu vyama vya siasa na wananchi kuwa na fursa ya kufanya maandamano, lakini aliizuia.

“Lakini Rais amevunja Katiba kuzuia vyama kufanya maandamano na mikutano ya hadhara. Kwa kweli hilo kama chama hatutalisahau,” alisema Matwange.

Katibu Mkuu wa NCCRMageuzi, Danda Juju alisema chama chake hakitasahu ukandamizaji uhuru na demokrasia uliofanywa na Serikali, vitu ambavyo vilipiganiwa tangu enzi za ukoloni ili kuwa huru kujiongoza.

“Hivi ni vitu ambavyo tumeviona katika utawala wa Rais Magufuli, amevikalia tena sana, tunakosa uhuru na demokrasia ambavyo tulivipigania,” alisema Juju. Alibainisha kuwa kutokana na hali hiyo, inaonesha kuwapo ukiukwaji mkubwa wa Katiba.

Naye Ofisa Habari wa ACTWazalendo, Abdalah Hamis kama vyama vingine, alisema kwa mwaka huu, hawatasahau tukio la kuminywa kwa demokrasia na kuvunjwa kwa Katiba kulikofanywa na Serikali.

“Kwa sababu mwaka 1992 baada vyama vingi kuruhusiwa, tuliruhusiwa kukutana na kufanya siasa kwa ajili ya kutafuta wanachama,” alisema Hamis.

Alisema mwaka huu ulianza kwa Serikali kupiga marufuku mikutano hiyo jambo ambalo alisema ni uvunjifu wa Katiba hivyo ACT haitasahau tukio hilo na kuomba lisiendelee mwakani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo