Mabaki ya faru John utata mtupu


*Yasemekana si rahisi kaburi Lake Kuonekana
*Mtaalamu ashauri itumike damu yake iliyopo

Fidelis Butahe

WAKATI wahifadhi wanyamapori wakieleza kuwa mkakati wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kumsaka faru John kwa kuchukua vinasaba hautafanikiwa kwa sababu hakuna kaburi lake, wataalamu wa wanyamapori na vinasaba wamesema kaburi si njia pekee ya kujua ukweli kuhusu kifo cha mnyama huyo.

Baadhi ya vyombo vya habari jana vilinukuu baadhi ya wahifadhi wakieleza kuwa hakuna kaburi la faru huyo, kwa kuwa hakuzikwa na kwa maana hiyo mpango wa kupima vinasaba utakwama.

Lakini, jana wataalamu hao waliieleza JAMBO LEO, kwamba kitu chochote kutoka kwa kiumbehai kinaweza kuchukuliwa na kupimwa vinasaba, huku wakisisitiza kuwa haiwezekani mnyama mkubwa kama faru afe miezi miwili tu kisha kusiwe na mabaki yanayoweza kuchukuliwa kama sampuli.

Ufafanuzi huo wa kitaalamu ulitolewa zikiwa zimepita siku tatu tangu Serikali ieleze kuundwa timu ya kuchunguza utaratibu wa kuhamishwa kwa faru huyo aliyeripotiwa kufa Agosti 18, kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwenda hifadhi ya Faru Weusi ya Sasakwa   iliyoko Grumeti.

Katika maelezo yake, Waziri Majaliwa alitaka kufukuliwa kwa kaburi la faru huyo anayeripotiwa kufa, kuchukua vinasaba vya masalia yake na kisha kwenda NCAA kuchukua vinasaba vya watoto wake na kuvilinganisha na pembe alizopelekewa kama ushahidi wa kifo hicho.

Majaliwa alitoa kauli hiyo licha ya Desemba 9 kupokea taarifa ya kuhamishwa kwa faru huyo, huku Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akisema alihamishwa kwa sababu ya kupunguza tatizo la kuzaliana ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.

Sakata hilo liliibuka Desemba 6 baada ya Waziri Mkuu Majaliwa akiwa ziarani Arusha, kuuagiza uongozi wa NCAA, kumletea nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru huyo kutoka kwenye hifadhi hiyo, ndani ya siku mbili.

Licha ya kuletewa taarifa hizo na kuelezwa kuwa mnyama huyo amekufa, Majaliwa alihoji aliumwa lini, daktari gani aliyemtibu na zilipo taarifa za matibabu yake na kuagiza mwili wa faru huyo ufukuliwe na kutazama kama vinasaba vyake vinaendana na watoto wake 26 ambao bado wako kwenye bonde la Ngorongoro.

Mmoja wa madaktari wa wanyamapori ambaye aliomba kutotajwa jina gazetini ili kutoathiri uchunguzi wa tukio hilo, alisema: “Yule ni mnyama wa porini, si binadamu. Akifa kinachoondolewa ni nyara za Serikali, si kubebwa na kuzikwa mahali, ila pale alipofia watu huamini ni kaburi.

“Huwezi kusema vinasaba vyake havipo, vinapatikana sehemu nyingi sana, kuna ngozi zinabaki pale (alipofia), mifupa. Si kwamba mnyama akioza anaisha kila kitu hapana. Ngozi ya faru ni ngumu sana na inabaki muda mrefu sana. Haiwezi kutoonekana kwa miezi miwili tu, hata na mifupa yake!”

Alisema kama ngozi ya tembo inaweza kukaa miaka miwili na bado alama zake zikabaki, haiwezekani ngozi ya faru ikatoweka kabisa tena ndani ya miezi miwili tu, “inaweza kukaa takribani mwaka mmoja.

“Bado kuna mabaki yake, hata umbile lake unaweza kuliona na kujua huyu faru amefia hapa, yule ni mnyama mkubwa si sungura, kwamba unaweza kumla na kutafuna mifupa yote,” alisema daktari huyo aliyeeleza anafanya shughuli zake kwenye mbuga mbalimbali nchini kwa hiyo anajua mambo mengi.

Daktari huyo alibainisha kuwa hata katika kumhamisha mnyama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, ni lazima achukuliwe damu, huku akihoji kuwa kama hata hiyo damu nayo haiwezi kupatikana.

“Mnyama yule amekufa, vinasaba vyake haviwezekani vikakosekana. Nafikiri Serikali inafanya vizuri, kila mtu awe macho, kwamba usifanye kitu ukajificha kichakani, wafanye uchunguzi ili kubaini ukweli. Hakuna mtu kufanya ujanja ujanja kama zamani,” alisisitiza.

Wakati mtaalamu huyo akieleza hayo, Dk Absalom Maiseri wa hospitali ya Lugalo, Dar es Salaam, alieleza jinsi ya kuchukua vinasaba kwamba, “wanachukua sampuli ya vitu vyote iwe manyoya, mate au mbegu za uzazi.

“Vinasaba viko ndani ya kina cha seli. Vinasaba ndio vimebeba chembe za urithi zenye maelekezo ya shughuli za mwili ikiwamo mwonekano wote.

Alisema pembe za faru John zinaweza kuchukuliwa sampuli na kulinganishwa na sampuli yoyote kutoka kwa watoto 26 wa mnyama huyo.

“Wahandisi wa vinasaba watachambua vinasaba vya pande zote mbili na kulinganisha kitaalamu, ikiwemo kutazama kama malighafi za chembe za urithi ndiyo hizo zilizopo kwa uzao wake (watoto wake),” alisisitiza.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo