John Banda, Dodoma
KITUO cha watu wenye ulemavu wa macho
cha Matembe Bora cha Buigiri wilayani Chamwino ambacho hujishughulisha pia na
kilimo cha bustani za mbogamboga, kimeiomba Serikali na taasisi kukipa wataalmu
kwa ajili ya elimu itakayowawezesha kuboresha kilimo chao ili kujiinua kiuchumi
zaidi na hatimaye waondokane na utegemezi.
Ombi hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti
wa Kituo hicho, Yarerd Chileso kwa niaba ya wenzake walipopokea msaada wa vifaa
vikiwamo nguo, sabuni viatu na mafuta ya kupaka kutoka Umoja wa Madhehebu ya Kikristo
Dodoma.
Chileso alisema kutokana na
kujishughulisha na kilimo cha mbogamboga kwa lengo la kujiinua kiuchumi
wameomba watalaamu hao wa kilimo ili wapate elimu ya kuboresha kilimo na
hatimaye kuongeza kipato na kujiinua kiuchumi.
“Sisi tulio hapa kituoni ni walemavu wa
macho, lakini pamoja na ulemavu huo tunajishughulisha na kilimo cha mbogamboga
kama vile mchicha, kabichi, nyanya, spinachi
na pilipili za kawaida na hoho, lakini hatuna utaalamu, hivyo tunaomba
wataalamu ili watuwezeshe kielimu zaidi,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kilimo hicho pia
kimekuwa kikiwawezesha fedha wanazopata kununua mahitaji ikiwa na pamoja kusomesha
watoto wao na matibabu.
Aidha, Mwenyekiti huyo alisema kupewa
watalamu hao kutawezesha kuachana na tabia ya ombaomba ambayo imekuwa ikifanywa
na baadhi ya wasiojiweza kwa kuwa tayari watakuwa wameonesha mfano kwa vituo
vingine vinavyotunza wenye mahitaji maalumu ili
kushiriki shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo, walemavu hao wakizungumza
kwenye hafla hiyo walimtaka Diwani wa Buigiri, Kenneth Yindi kuwasiliana na Serikali
ili wawekewe alama za barabarani kutokana na kituo chao kuwa karibu na barabara
kuu ya Dodoma - Morogoro ili wavuke kwa usalama zaidi.
Diwani Yindi alisema tatizo la alama za
barabarani linatakiwa kushughulikiwa na tayari taarifa zimetolewa kwa kuanzia
ngazi ya wilaya hadi Taifa.
0 comments:
Post a Comment