Familia ya Malecela yatoa neno


Charles James

Anne Kilango Malecela
WAKATI habari za kutumbuliwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba na Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk. Mwele Malecela, zikiuteka mwaka 2016 kutokana na wote kutokea familia moja, wenyewe wameibuka na kutoa neno.

Dk. Mwele ambaye alikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliojitosa kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa na chama hicho kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, alilieleza JAMBO LEO kuwa anasita kueleza kiundani kuhusu uteuzi wake kutenguliwa kwa sababu anachokieleza huchukuliwa tofauti.

“Naomba uniruhusu nisiongee chochote kwa sababu tangu uteuzi wangu utenguliwe kila ninachoongea kimekuwa kikichukuliwa negative (mtazamo hasi), hivyo naomba uniache tafadhali,” alisema Dk. Mwele.

Kutumbuliwa kwa Kilango ambaye ni mke wa Waziri Mkuu mstaafu John Malecela pamoja na mwanaye, Mwele kuliibua maswali juu ya nini kilichoikumba familia hiyo ambayo mwaka 2016 umeshuhudia wanafamilia hao wakiondolewa katika nyadhifa zao.

Desemba 16 mwaka huu, Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa Dk Mwele baada ya kutoa ripoti ya mwaka ya taasisi hiyo iliyoonyesha kuwa watu 80 waliofanyiwa utafiti waligundulika kuwa na virusi vya homa ya zika.

Taarifa ya utafiti huo ilionyesha kuwa kati ya watu 533 waliopimwa, 83 (asilimia 15.6) walikuwa wameambukizwa virusi vya homa ya zika, Pia, kati ya watoto wachanga 80 waliozaliwa na ulemavu wa aina mbalimbali, asilimia 43.8 walikuwa wameambukizwa virusi vya homa ya zika.

Uteuzi wa Kilango ulitenguliwa siku 27 baada ya kuapishwa Ikulu Dar es Salaam. Mbunge huyo wa zamani wa Same Mashariki aliondolewa katika nafasi hiyo baada ya kudai kuwa mkoa wake hauna watumishi hewa, lakini baada ya uchunguzi kufanyika ikabainika kuwa kuna watumishi hewa 45.

Agizo la kutaka wakuu wa mikoa kusaka watumishi hewa lilitolewa na Rais huyo wa Awamu ya Tano wakati wasaidizi wake hao wakiapa. Ilisemekana kuwa licha ya Kilango kueleza kutokuwa na watumishi hewa ilibainika kuwa kiasi cha Sh. milioni 339 kilikuwa kimelipwa bila kuelezwa kina nani walilipwa.

“Nimejiuliza sana, nikajiuliza sana na kwa kweli nikajiuliza sana kwa masikitiko, kwanini Mkuu wa Mkoa alisema hakuna watumishi hewa,” alisisitiza
Rais Magufuli katika taarifa yake ya kutengua uteuzi wa Anne Kilango.

Lakini jana Kilango alipoulizwa kuhusu hatua hiyo sambamba na yaliyoikuta familia hiyo alisema swali hilo hakupaswa kuulizwa jana kwa sababu alikuwa katika Sikukuu ya Krismasi.

“Mimi nipo kwenye Krismasi naandaa pilau la sikukuu, naomba uniache,” alisema Kilango.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo