Abraham Ntambara na Hussein Ndubikile
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC) kimefungua shauri msingi la kikatiba kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Dar es Salaam kuomba tafsiri ya kisheria dhidi ya ongezeko la makato
ya asilimia 15 kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu nchini.
Akizungumza na wanahabari jana Dar es
Salaam baada ya kufungua shauri hilo, mmoja wa mawakili, Dickson Matata alidai
katika shauri hilo namba sita la mwaka 2017
kituo hicho kinaiomba Mahakama kutoa tafsiri ya kifungu kidogo cha 20
(b) cha Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini (HESLB).
Wakili Matata alisema katika shauri hilo,
walalamikiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Bodi ya Mikopo ambapo
alibainisha kuwa wakati wanafunzi wanaingia mikataba na Bodi hiyo, ongezeko hilo
halikuwapo hivyo kuanza kukatwa ni kinyume na sheria.
"Tunacholalamikia ni kwamba wakati
wanakopa, wakopaji wengi ambao wamenufaika na mikopo ya HESLB walikopa lakini
kiwango wanachotozwa kwa sasa hasa baada ya kufanyika kwa marekebisho ya sheria
hiyo mwaka jana, ni kikubwa ikilinganishwa na mishahara wanayopata,"
alisema Wakili Matata.
Alibainisha kuwa kibaya zaidi ni kwamba
sheria hiyo inaanza kuathiri hata walioingia mkataba kabla ya ongezeko huku
akiongeza kuwa kwa mujibu wa sharia, inatakiwa kuanza kwa wanaoingia mkataba
mpya na Bodi hiyo.
Mlalamikaji wa shauri hilo, Shukuru
Mlwafu alisema si kwamba wanapinga kurejesha mikopo hiyo, bali ni kutaka
utaratibu uliowekwa ufuatwe.
"Mimi ni mlipaji mzuri tu na hadi
sasa nimeshalipa Sh milioni nne, lakini hatuwezi kulipa kinyume na sharia, kwa
sababu tulichukua kwa utaratibu na lazima turudishe kwa mujibu wa taratibu za
kisheria," alisema Mlwafu.
0 comments:
Post a Comment