Julieth Peter, Manyara
Joel Bendera |
MKUU wa Mkoa wa
Manyara, Dk Joel Bendera, amesema kuna umuhimu kwa wadau wa kahawa
kutathimini kwa kina matatizo yanayolikabili zao hilo Manyara, Arusha na Kanda
ya Kaskazini na kupendekeza hatua za msingi za kuchukuliwa.
Dk Bendera alisema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa zao la kahawa kwa Kanda ya Arusha na Manyara, uliofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara akitaka hatua hizo ziainishe zinatekelezwa na nani.
Alisema kabla ya
kuanguka kwa kilimo cha kahawa, kilikuwa miongoni mwa shughuli kuu zilizowaingizia
wananchi kipato kikubwa, kilichowezesha kusomesha watoto wao, kuboresha
makazi yao, kujipatia fedha kwa chakula na mahitaji mengine muhimu ya
maendeleo.
“Umuhimu wa kahawa
si kwa mikoa inayolima bali ni kwa Taifa zima kwani inachangia kuliingizia
fedha nyingi za kigeni ikiwa mojawapo ya mazao makuu ya asili ya biashara ambalo
linachangia wastani wa asilimia tano ya thamani ya mauzo ya
bidhaa nje na asilimia 24 ya thamani ya mauzo yanayotokana na mazao ya
asili,” alisema.
Alisema pamoja na kwamba kilimo cha kahawa ndiyo shughuli kuu zilizokuwa zinawaingizia wananchi kipato kikubwa, kilimo hicho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto nyingi zilizojitokeza na kutishia maendeleo ya kilimo cha kahawa nchini.
Dk Bendera
alisema kuporomoka kwa uzalishaji wa kahawa kulisababishwa na
kuyumba kwa bei na wakulima kukata tamaa ya kutunza mashamba
yao, ukosefu wa pembejeo za uhakika, magonjwa na wadudu
wanaoshambulia kahawa.
Alitaja
changamoto zingine kuwa ni mibuni kuwa na umri mkubwa, kupungua kwa
rutuba ya udongo kutokana na kilimo cha muda mrefu kisichozingatia
kanuni za kilimo bora, mabadiliko ya tabianchi
yaliyosababishwa na uharibifu wa mazingira na kuathiri kilimo
cha mazao ikiwamo mibuni.
Pia, uzalishaji na
tija ndogo kutokana na wakulima wadogo kutozingatia kanuni za
kilimo cha mazao mengine.
“Kuyumba kwa
ufanisi wa kilimo cha mibuni kwenye kanda yetu kumeleta madhara makubwa
katika vita yetu ya kuondoa umasikini na pia kumeathiri uchumi wa
kanda yetu,” alifafanua Dk Bendera.
Aliwasisitiza
wadau wa kahawa wa Kanda ya Kaskazini, kujadili kwa kina baadhi ya matatizo ya
msingi ambayo yamekuwa yanakwamisha maendeleo ya kahawa na kuyapatia
ufumbuzi yaliyo ndani ya uwezo wao kama wadau.
Hata hivyo,
alisema kuongezeka kwa uzalishaji wa kahawa ni lazima kuende sambamba na upatikanaji
wa soko la uhakika na kufafanua kuwa soko la kahawa ni pamoja na kuhamasisha
soko la ndani kwa matumizi ya kahawa bidhaa zake.
0 comments:
Post a Comment