Mwandishi Wetu
SERIKALI ilianza kutatua changamoto ya migogoro
ya ardhi mkoani Morogoro kwa kuwa ndio ulikuwa umekithiri
kuliko mingine nchini, imeelezwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula akijibu swali
la nyongeza la Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM) lililohoji sababu
za Serikali kuanza kazi hiyo mkoani humo, licha ya kuwa tatizo hilo liko karibu
mikoa yote.
Akifafanua, Mabula alisema migogoro ya
ardhi Morogoro ilikuwa mingi tofauti na mingine hivyo wakaamua kuanzia huko ili
baadaye mikoa iliyobaki.
Swali hilo la nyongeza lilitokana na
swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Makiragi (CCM) lililohoji
namna Serikali ilivyojipanga kupima ardhi ili kuondokana na migogoro nchini.
Wakati akijibu swali hilo, Mabula
alisema azma ya Serikali ni kuhakikisha programu ya kupanga na kupima ardhi inafanyika
ili kuhakikisha migogoro inapungua, kuwezesha wananchi kutambua maeneo yao na
kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Hiyo itahusisha halmashauri 181 kwa
miaka 10 na itafanyika kwa awamu mbili za miaka mitano mitano na mikoa
iliyobaki itawekwa kwenye ratiba hiyo,” alisema.
0 comments:
Post a Comment