Wahoji wanasiasa kuachwa kwenye vyeti feki


Fidelis Butahe na Hussein Ndubikile

Julius Mtatiro
WAKATI watumishi na viongozi wa umma 9,932 wakipoteza ajira zao kwa madai ya kughushi vyeti, wanasiasa nchini wamekosoa kitendo cha mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya kuachwa kwenye uhakiki huo ulioacha vilio na simanzi maeneo mbalimbali nchini.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema haki hutolewa kwa watu wote si kundi fulani pekee huku Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro, akienda mbali zaidi na kueleza ugumu wa kutenganisha dhana ya siasa na utumishi wa umma kwa mawaziri, wabunge, wenyeviti wa vijiji na madiwani.

“Hawa wenye vyeti feki haikupaswa kuwafukuza. Kwanza, ilitakiwa kuangalia miongoni mwao je wapo walioonesha weledi kazini? Nasema hivi kwa sababu wapo wenye cheti feki cha kidato cha nne, lakini wana Shahada na ni watendaji wazuri,” alisema Mtatiro.

“Pia wapo madaktari bingwa wenye vyeti feki vya kidato cha nne, lakini kwa sasa wanaaminika sana, sasa huyu unamfanyaje. Unamfukuzaje huyu?”

Takribani wiki moja iliyopita Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki alikabidhi majina ya watumishi hao kwa Rais John Magufuli baada ya kuvifanyia uhakiki vyeti vyao kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.

Alisema uhakiki huo haukugusa viongozi wa kisiasa wakiwamo mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na madiwani.

Wakati Kairuki akisema watu hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua pamoja na mawakala wanaotumika kutengeneza vyeti, Rais Magufuli aliagiza waondoke kazini wenyewe na kunyimwa mishahara yao ya Aprili.

Kati ya watumishi 400,035 waliofanyiwa uhakiki wa vyeti vya kidato cha nne, sita na ualimu waliopatikana wakiwa safi ni 376,969 sawa na asilimia 94.2.

Katika maelezo yake, Mtatiro alisema: “Kwanza kwa dhana ya uanzishwaji wa wakuu wa mikoa na wilaya hawa si wanasiasa, ni watumishi wa umma. Wanasiasa katika Serikali wapo wa aina nne; kwanza kuna rais, makamu wake na  waziri mkuu, pili ni mawaziri, tatu ni  wabunge na nne ni madiwani,” alisema Mtatiro.

“Huwezi kutenganisha dhana ya siasa na utumishi wa umma kwa mawaziri, wabunge, wenyeviti wa vijiji na madiwani. Hawa wote ni watumishi wa umma kwa sababu wanalipwa mishahara na fedha za umma.”

Alisema kwa kuwa wote ni watumishi wa umma, haiwezekani ufanyike uamuzi wa kubaini vyeti feki halafu baadhi ya watu waachwe.

Alibainisha kuwa vita dhidi ya vyeti feki ilipaswa kumulika wanasiasa, kama ni wabunge taarifa zao zifuatiliwe kubaini waliodanganya elimu zao.

“Hii ilipaswa kuanzia juu na watakaobainika kuonywa na kuchukuliwa hatua. Iweje uanze na kada ya chini ya utumishi wa umma na kuacha kada ya juu ya utumishi wa umma? Hili ni jambo lisilokubalika, tunapongeza ila hatua zinazochukuliwa ndizo tunazopinga,” alisema.

Alisema Rais mzuri anaweza hata kutembelea majambazi walioshindikana gerezani na kusisitiza kuwa ni ajabu kuona Rais akisema watu walio magerezani si raia wake, kwa sababu tu ya makosa yao na kufananisha jambo hilo na watumishi wa umma waliofukuzwa kwa vyeti feki huku wengine wakiachwa kwa kigezo cha uanasiasa.

Alisema watendaji wa aina hiyo walipaswa kuandaliwa programu maalumu ili kurudia kidato cha nne na kupata cheti halali au kuachishwa kazi kwa maslahi ya umma, ikiwa ni pamoja na kulipwa mafao yao yote.

“Wapo walioitumikia Serikali kwa miaka 30, mtu huyu unamfukuzaje hivi hivi. Si bora wapewe likizo ya miaka miwili na kulipwa nusu mshahara ili wakasome na kupata cheti cha kidato cha nne,” alisema.

Akimtolea mfano mteule wa Rais ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mtatiro alihoji: “Huyu alifeli kabisa sasa mbona mpaka leo yupo huku wengine wakiondolewa?”

Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima (AFP), Rashid Rai alisema: “Hili jambo si sawa hata kidogo. Kughushi vyeti hakupaswi kuangalia hadhi ya mtu. Awe waziri, mbunge au mtu wa kawaida kama ana cheti feki anapaswa kuchukuliwa hatua tu.

“Kama sifa kwa wanasiasa inaelezwa kuwa ni kusoma na kuandika, mbona katika uombaji kazi, mfano wabunge wanataja mpaka shahada walizonazo? Huu ni uongo wa mchana kabisa, ni sawa na dhambi za wizi, uwe mdogo au mkubwa ni wizi tu.”

Tofauti na Mtatiro, Rai alisema kuliko kuwapa muda maalumu warudie kidato cha nne, ni bora wafukuzwe kazi na kuchukuliwa hatua.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema: “Nitalizungumzia kwa kina kwenye hotuba ya elimu wakati nawasilisha maoni ya upinzani kuhusu bajeti ya Wizara ya Elimu, nitaweka vielelezo na kuanika udhaifu mkubwa katika hili.”

Katibu Mkuu wa National League for Democracy (NLD), Tozy Matwanga alisema uamuzi wa Rais ni mzuri na kumwomba uhakiki huo ufanyike kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge na mawaziri.

"Watumishi hawatakiwi kuwa na doa la kitaaluma, maana madhara yake ni utendaji mbovu usioridhisha. Kuwaacha baadhi kunaweza kuitia doa Serikali kwa wananchi na kuanza kuhisi kuna viongozi wanalindwa akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ana cheti feki,” alisema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu alisema udhaifu wa kukagua vyeti vya watumishi unasababishwa na Rais kuhodhi madaraka makubwa kwa mujibu wa Katiba.

"Watumishi wa umma wengi wanateuliwa na Rais, kila rais ana vigezo vyake, achilia hiyo Katiba inayompa madaraka ya kuwateua kwa kigezo cha kujua kuandika na kusoma," alisema Profesa Baregu.

Mjumbe huyo wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema Tume hiyo ilitoa rasimu ya Katiba iliyopunguza madaraka ya rais katika uteuzi wa mawaziri, wabunge, wakuu wa wilaya, mikoa na madiwani.

“Katika rasimu tulipendekeza uteuzi huo ufanywe na Tume ya Utumishi wa Umma,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo