*Ni kwa adhabu ya kuzuiwa vikao vya Bunge la Bajeti
*Asamehewa kwa
kuonesha kujirudi, kumrudia Mungu
Sharifa Marira, Dodoma
SAA chache baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka
ya Bunge kupendekeza Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) azuiwe kuhudhuria
vikao vyote vilivyobaki vya Bunge la Bajeti, wabunge bila kujali itikadi za
vyama vyao wamemnusuru kwa kumwombea radhi.
Mbali na Mdee, wengine waliotiwa hatiani na Kamati hiyo
ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Mbunge wa Bunda, Esther
Bulaya, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander
Mnyeti ambao wote walisamehewa baada ya kuomba radhi kwa makosa waliyofanya.
Katika uamuzi uliosomwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati
hiyo, Almas Maige, Kamati ilimtia hatiani Mdee kwa tabia yake ya mara kwa mara
ya kudharau Mamlaka ya Spika na kutoa lugha ya matusi na kuudhi kama ilivyotokea
katika mkutano wa kuchagua wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alisema ni
muhimu viongozi kuwa na unyenyekevu na kwamba jambo la msingi katika uamuzi wa
Kamati ni kusamehe walioomba radhi.
“Ukitaka kuadhibu mtoto, akiomba radhi unamsamehe, kwani
unapata ushahidi kwamba alilofanya limesamehewa. Naomba niwaombee radhi
Mdee na Bulaya, kwani licha ya kuomba radhi ndani ya Kamati pia Mdee alikuja
mbele ya Bunge kuomba radhi na kuonesha kujutia alichokifanya, siku hiyo kuna
mbunge wa CCM alisema Mdee ameokoka kama ishara kwamba amebadilika,’’ alisema
Selasini.
Alisema Mdee aliomba radhi kwa wapiga kura wake, Spika, wabunge
na Watanzania kwa ujumla akionesha kujutia alichokifanya cha kumtukana Spika na
kuahidi kutorudia.
Alisema wabunge wote ni waumini wa dini na wanafundishwa
kusamehe hivyo kutokana na unyenyekevu alioonesha Mdee ndani ya Bunge na kwenye
Kamati, anastahili kuunganishwa na wenzake ambao waliomba msamaha wakasamehewa,
kwani kwa kufanya hivyo wataonesha ni viongozi ambao wanaweza wakaguswa na
wakarudi kuwa kitu kimoja.
Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Shahari Mngwali (CUF) alisema:
“Kuna semi nyingi kwenye jamii yetu ya Kiswahili, kama; ‘mtoto akinyea mkono
haukatwi’ na dini zetu zinatutaka tutoe adhabu zinazofundisha kuliko
zinazoumiza, pia kusamehe kuna matokeo mema zaidi, si duniani tu hata siku za
mwisho.’’
Alisema anapongeza alilofanya Mdee la kuomba radhi
hadharani, kwani alisimamia busara za kumeza kiburi cha kibinadamu na kuamua
kujishusha, jambo ambalo lilitoa picha nyingine ya maisha yake.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alisema Kamati ilifanya
kazi iliyoagizwa vizuri, lakini kuna upungufu kwenye ripoti, kwani zipo dalili
za kigugumizi katika mapendekezo.
“Inawezekana baadhi ya watuhumiwa wakawekwa kwenye kundi
la kuhukumiwa na wengine wakasamehewa, ndizo dalili za kigugumizi,” alisema.
Alisema Bunge lina wabunge waungwana, lakini wakati
mwingine ndimi zao zinatekeleza na ili kufungua ukurasa mpya na hasa maneno ya
Mdee amegusa wengi alipoamua kumtanguliza Mungu.
Alisema Mdee alipiga hatua kubwa, kama ameanza
kumtanguliza Mungu na kumwomba amwongoze kwani Mdee anayefahamika si huyo na
pia karipio alilopewa Bulaya ni adhabu, hivyo pia afutiwe kwani ameanza
kujirekebisha kama ambavyo Kamati ilikiri.
“Niwakumbushe tu watu, kwamba Bunge hili unapolikosea
unatakiwa uombe radhi kabla halijawekwa tishio lolote la kuchukuliwa hatua,
kwani kuanza kulialia ukishaitwa kwenye Kamati si sawa,” alisema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana
na Walemavu, Jenista Mhagama aliomba kutengua kanuni ili adhabu iliyokuwa
imewekwa awali dhidi ya Mdee ya kutohudhuria vikao vyote vya Bunge la Bajeti
ifutwe na kusamehewa, ila kwa masharti ya kutorudia kosa ndani ya kipindi chote
cha Bunge na kwamba akifanya hivyo atatakiwa kutekeleza adhabu hiyo bila kuitwa
na kikao chochote.
0 comments:
Post a Comment