Leonce Zimbandu
MKAZI wa Kipunguni, Ilala, Obadia Mtawa,
amemtelekeza mkewe, watoto wanne na kwenda kusikojulikana kutokana na ugumu wa
maisha.
Tukio hilo lilifahamika baada ya Nuru
Khasim kuzungumza na mwandishi wa gazeti hili jana kuhusu mumewe huyo
kumtelekeza na kutoweka na yeye kutangatanga na watoto.
Alisema ni mwaka mmoja sasa tangu Mtawa
aikimbie familia yake, hivyo anaendelea kuteseka huku akikosa msaada wa ndugu
kutokana na tabia mbaya ya ndugu yao.
“Nimevumilia kwa muda mrefu kwani siku
moja wakiwa na rafiki yake walininyonga mkono na kuvunja kijiti nilichoweka mwilini
kuzuia kushika mimba,” alisema.
Alisema baada ya ukatili huo
alilazimishwa kufanya mapenzi na kushika ujauzito na kujifungua kwa njia ya
operesheni na kukosa msaada kwa vile mumewe alitoweka.
Aliongeza, kuwa kutokana na hali ya
maisha kuwa ngumu, alikwenda ofisi ya Serikali ya Mtaa ya Kipunguni kulalamika ili
kupata msaada wa malezi.
Ofisa Msaidizi wa Ustawi wa Jamii
Kipunguni, Clement Sinda alisema ofisi
hiyo ilipokea malalamiko ya Nuru, na inaendelea kutafiti kwa kushirikiana naye
ili kumpata mumewe.
“Tunahitaji kupata taarifa za eneo
analoishi sasa ili iwe rahisi kufanya mawasiliano na ofisa ustawi wa jamii wa
eneo hilo, ili akamatwe na kurudishwa Dar es Salaam,” alisema.
Alisema
ofisi hiyo inaendelea pia kumtafuta rafiki wa Mtawa aliyeshiriki kumpiga na kumnyonga
mkono Nuru na kuvunja kijiti alichoweka cha uzazi wa mpango.
Mwandishi wa habari hizi alipompigia
simu Mtawa huku akisita kutaja anakoishi, alisema alitoweka Dar es Salaam
kutokana na ugumu wa maisha na yuko Morogoro akijishughulisha na kilimo.
“Sijamtelekeza, bali ni ugumu wa maisha,
tayari nimelima mpunga na mahindi, nitarudi kuchukua familia yangu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment