Mary Mtuka
Deogratius Kwiyukwa |
SHIRIKA la Posta Tanzania limeanzisha
vituo vya kisasa vitavyotoa huduma jumuishi za kimtandao kwa jamii.
Aidha, limepata Mkurugenzi Mtendaji mpya
atakayekuwa pia Postamasta Mkuu, Deogratius Kwiyukwa, nafasi ambayo awali
ilikuwa ikishikiliwa na Fortunatus Kapinge ambaye anatarajia kustaafu hivi
karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar
es Salaam jana, Mkurugenzi huyo mpya alisema katika kuhakikisha upatikanaji wa
huduma bora kwa jamii kuna haja ya shirika kwenda na wakati kwa teknolojia ya
kisasa ili kufikia wateja haraka.
Kwiyukwa alitaja huduma zinazotolewa kwa
mtandao kuwa ni za uwakala wa malipo ya gawio ya kampuni, mifuko ya hifadhi ya
jamii ili kurahisisha malipo ya wastaafu, malipo ya Baraza la Mitihani, uwakala
wa benki na ulipaji kodi zikiwamo za TRA na huduma za Posta.
Alisema kuna kila sababu ya kuboresha
mfumo wa shirika hilo ili kuwapunguzia wananchi usumbufu wa kufuata huduma za
mtandao maeneo tofauti.
"Ni takribani wiki mbili tangu nianze
kazi, lakini kama kiongozi nitahakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wateja
wetu kwani hiyo ndiyo njia pekee kwa kila mfanyakazi," alisema Kwiyukwa.
Alisema shirika linawajibika kuhakikisha
teknolojia mpya na huduma za kisasa za kiuchumi na kijamii zinafikia watu wengi
zaidi katika maeneo ya vijijini na mjini ambapo kwa Dar es Salaam wamefikia
kata 32.
Aliongeza kuwa shirika limeweka msukumo
na ushawishi maalumu katika uazishaji vituo ili kuwezesha huduma za utawala serikalini
kufanyika katika sehemu moja ikiwa ni pamoja na upimaji wa maduhuli, kodi na
ada katika uendeshaji wa shughuli za Serikali yao.
0 comments:
Post a Comment