Suleiman Msuya
Julius Mtatiro |
SERIKALI imeshauriwa kuzingatia haki, usawa
na sifa zinazokubalika kwa watumishi wote wa umma ili kuepusha dhana ya ubaguzi
baina yao.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa
Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) Julius Mtatiro na Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana kwenye
kipindi cha Mizani ya Wiki cha Azam TV kuhusu kufukuzwa watumishi wa umma 9,932
kwa kughushi vyeti.
Mtatiro alisema iwapo hakutakuwa na
usawa kwa watumishi wote ni dhahiri kuwa hakutakuwa na majungu na malalamiko
baina ya watumishi.
Alisema mchakato wa Serikali kubaini
watumishi wenye vyeti vya kughushi ni hatua ya kupongezwa ila isibague baadhi
ya makundi katika utumishi wa umma.
”Hatua hizi zinaungwa mkono na mtu yeyote
anayependa haki na uwazi ila utaratibu uliofanyika unaacha maswali, mbona
hakuna usawa nadhani hapa tunapaswa kuangalia upya,” alisema.
Mwenyekiti huyo alishauri kuwa iwapo
haki itatendeka, hakuna mtu ataibuka na kulalamika huku akisisitiza wahusika
wapewe mafao kwani wametumikia nchi.
Alisema miaka 20 hadi 30 ya utumishi wa
wafanyakazi hao unapaswa kuthaminiwa, hata kama walifanya makosa kupata elimu
kwani nia yao haikuwa mbaya.
Dk Bana alisema taarifa hiyo imeiamsha
nchi, hivyo ni vema kuangalia mfumo mzima wa elimu na utumishi wa umma kwani
haikubaliki.
Alisema utumishi unazingatia maadili na
miiko, hivyo kinachoonekana ni mifumo kuwa dhaifu, hali inayoruhusu watu
kufikiria kujihusisha na mambo yasiyokubalika kisheria.
“Nadhani mfumo unapaswa kuangaliwa,
kwani wakati mwingine unachochea jamii kujihusisha na kughushi vyeti, ni vema
kujitathmini upya kwa maslahi ya nchi,” alisema.
Aidha, alisema uamuzi wa Rais John
Magufuli kutangaza wafanyakazi 9,932 kufukuzwa kazi, unaweza kuwa wa hasira,
hivyo angepaswa kushauriwa njia ya kuchukua kabla ya kufika huko.
Alisema baadhi ya watumishi walibainika kuonesha
ufanisi mkubwa katika utumishi wa umma, hali ambayo inaacha maswali mengi nini
kiliwasukuma kufanya hivyo.
Bana alisema Serikali ina wajibu wa
kuendelea kuboresha utumishi wa umma ili kuzingatia maadili mema kwa maslahi ya
nchi.
Alisema kundi hili lilijitokeza kutokana
na udhaifu ambao umekuwapo kwa muda mrefu, hivyo iwe maandalizi ya mwanzo mpya
wa utumishi kurejea heshima yake.
0 comments:
Post a Comment