Benedict Liwenga
Harrison Mwakyembe |
WAZIRI wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ametaka vijana kutumia muda wao kujenga
utamaduni wa kujisomea vitabu badala ya kupoteza muda kwenye mitandao ya
kijamii kwa kuwa kusoma vitabu ndiyo msingi mzuri wa elimu.
Kauli hiyo aliitoa juzi
Dar es Salaam alipozindua kitabu cha “Colour of Life” kilichoandikwa na Ritha
Tarimo ambapo alisisitiza vijana kupenda kusoma vitabu ili kukuza elimu
yao.
Dk Mwakyembe alisema
baadhi ya vijana siku hizi hutumia muda wao mwingi kwenye mitandao ya kijamii
badala ya kujisomea, hivyo akashauri wajifunze kutoka kwa mwandishi wa kitabu
hicho ili kuwa waandishi hodari wa kutegemewa na Taifa.
Sambamba na rai hiyo,
Waziri Mwakyembe alimpongeza Ritha kwa juhudi zake kubwa na maarifa katika
kutunga na kuandika kitabu hicho ambacho alisema ni kizuri na chenye maudhui
mazuri kwa vijana hususan wanafunzi, hivyo kuitaka jamii kumuunga mkono kwa
kukisoma ili ipate kuelimika.
“Ukimkuta mtu kama Ritha anaandika
kitabu kipindi hiki ambacho vitabu vinaonekana kuondolewa kwa sababu ya
teknolojia, ni vema kumpa moyo na kumuunga mkono, kwa kuwa ametuonesha
Watanzania kuwa tunaweza, na kitabu hiki niwaambie ukweli, kina maudhui ya
kumtia moyo kijana kutokata tamaa ya maisha,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema Serikali inaunga
mkono juhudi za uandishi wa vitabu vyake na alichukua baadhi ya nakala za
kitabu hicho ili kuzipelekeka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ili
kuona namna kitabu hicho kinavyoweza kuisaidia jamii.
Ritha aliishukuru Serikali
kwa kukubali mwito wa kizindua kitabu chake na pia utayari wa Serikali kumuunga
mkono ili uandishi wake uwe wenye tija kwa Watanzania.
Alieleza kwamba,
kazi ya uandishi aliianza muda mrefu na sasa amepata nafasi ya kuungwa mkono na
Serikali na Watanzania ikiwamo familia yake na hatimaye kukamilisha kitabu
hicho na kukizindua rasmi.
“Nakushukuru Waziri kwa
kutumia muda wako kuja kuzindua kitabu hiki, nakushukuru sana na sasa naamini
ndoto zangu zinatimia, kitabu hiki nimekitengeneza kwa umbo dogo ili kiweze kuvutia
watu wengi kwani kina maudhui mazuri kwa vijana na jamii nzima ya kitanzania,”
alisema Ritha. ‘Colour of Life’ ni moja ya vitabu saba
alivyoandika Ritha.
0 comments:
Post a Comment