Grace Gurisha
UPANDE wa Serikali katika kesi ya Yusuf Yusuf ‘Mpemba’ (34)
anayetuhumiwa kwa ujangili, leo unatarajiwa kumsomea maelezo ya mashahidi pamoja
na wenzake, baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.
Maelezo hayo yatasomwa mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria
Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa sababu awali
upande huo ulidai kuwa wanajiandaa kuwasomea maelezo hayo.
Wakili wa Serikali, Elia Athanas alieleza hayo Dar es
Salaam baada ya upelelezi kukamilika.
Alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa kutajwa na pia kuna
maelezo yaliyochapwa yamerudishwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es
Salaam, kwa sababu maelezo hayo yametofautiana na maelezo halisi, hivyo
wanatakiwa wafanye marekebisho.
Alidai licha ya upungufu huo, lakini bado wanajiandaa
kuwasomea maelezo ya mashahidi washitakiwa wote.
Mbali na Mpemba ambaye ni mkazi wa Tegeta washitakiwa
wengine ni Charles Mrutu (37) wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa (40) wa
Mbagala Chamazi, Jumanne Chima (30) wa Mbezi, Ahmed Nyagongo (33) dereva na
Pius Kulagwa (46).
Washitakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na mtandao wa
ujangili na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6.
Ilidaiwa kuwa katika tarehe zisizofahamika kati ya Januari,
2014 na Oktoba, mwaka jana wakiwa maeneo tofauti ya Dar es Salaam, Tanga,
Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza
nyara za Serikali vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola za
Marekani 180,000 sawa na Sh milioni 392.8 mali ya Serikali bila kuwa na kibali
cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Aliendelea kudai kuwa katika mashitaka ya pili, Oktoba 26
mwaka huu, washitakiwa wakiwa Mbagala Zakhem ndani ya wilaya ya Temeke
walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 13.85 vyenye
thamani ya dola 30,000 sawa na Sh milioni 65.4.
Ilidaiwa kuwa katika mashitaka ya tatu, Oktoba 27
washitakiwa wakiwa Tabata Kisukulu walikutwa na vipande vinne vya meno
hayo vyenye uzito wa kilo 11.1 vyenye
thamani ya dola 15,000 sawa na Sh milioni 32.7, ambapo pia Oktoba 29 walikutwa
na vipande 36 vyenye thamani ya Sh milioni 294.6 bila kibali cha Mkurugenzi wa
Wanyamapori.
0 comments:
Post a Comment