Saidi Meck Sadik |
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Meck Sadik, amewataka waajiri kutekeleza
wajibu wao wa kuwapa wafanyakazi stahiki zao kwa mujibu wa kanuni na taratibu
za kazi.
Kauli hiyo
aliitoa jana wakati akitoa salamu za mkoa huo katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi
Duniani ambayo kitaifa yalifanyika mkoani humo.
“Waajiri
wanatakiwa kutenda haki kwa wafanyakazi. Wanatakiwa kuwapa wafanyakazi stahiki
zao kwa maana hiyo wanatakiwa kutekeleza wajibu wao huo,” alisema Sadik.
Alibainisha kuwa katika
mkoa huo wafanyakazi wamekuwa wakifanya kazi kwa ufanisi kutokana na kufahamu vema
falasafa ya Serikali, akisema hiyo inathibitika kutokana na kutoendekeza
maandamano.
Mkuu wa Mkoa alimwomba
Rais John Magufuli asaidie kuhakikisha viwanda ambavyo havifanyi kazi mkoani
humo vinafufuka ili kuongeza ajira kwa vijana.
Alieleza kuwa Kilimanjaro
ilikuwa na viwanda vingi vilivyokuwa vikitoa ajira nyingi kwa wananchi, lakini
sasa havifanyi kazi na kubainisha kuwa vipo ambavyo viliuzwa, lakini hadi leo
havifanyi kazi.
“Suala la viwanda
mkoani Kilimanjaro, wewe (Rais) ni shahidi, Moshi kulikuwa na viwanda vingi, vilikuwa
vinatoa ajira zaidi ya 10,000, vyote vimekufa, vijana wanazurura bila ajira,”
alisema Sadik.
Alisema kwa kuwa Rais
amedhamiria kufufua viwanda, ni vema asimamie suala hilo ili vianze uzalishaji
na vijengwe vingine vipya ili kuondoa tatizo la ajira.
Aidha, aliwataka
wakazi wa mkoa huo kujenga viwanda mkoani kwao kwa kuwa wana fedha za kutosha badala
ya kujenga mikoa mingine ambako alieleza kufanya hivyo kutasaidia kuleta
maendeleo.
0 comments:
Post a Comment