Maeneo mengi nchini yajengwa holela


Joyce Kasiki, Dodoma

Angelina Mabula
ASILIMIA 67 ya maeneo yaliyojengwa kwenye miji saba na manispaa Tanzania Bara na Zanzibar yapo kwenye kiwango cha ujenzi holela, Bunge limeelezwa.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, aliliambia Bunge jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza (Chadema).

Awali katika swali lake, Peneza alitaka kujua mkakati wa Serikali kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora kwa kuwa kumekuwepo na tatizo la makazi duni na kusababisha afya mbovu na hivyo kupunguza nguvu ya uzalishaji.

Akijibu swali hilo, Mabula alisema, ripoti ya hali halisi ya miji nchini iliyoandaliwa na Mtandao wa Miji Nchini ya mwaka 2014 ilibainisha wastani wa kiwango cha ujenzi holela kwenye miji hiyo kuwa ni asilimia 67.

“Mengi ya maeneo hayo hayana miundombinu na huduma za msingi kama vile maji safi na salama, barabara na mifereji ya maji ya mvua na udhibiti wa majitaka na taka ngumu.”

Alisema hali hiyo husababisha mafuriko, milipuko ya magonjwa, mazalia ya mbu na nzi na mandhari mbaya ya kuishi inayosababisha afya duni na kupunguza nguvukazi.

Hata hivyo, alisema Serikali imeandaa programu na mikakati ya kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na programu ya kitaifa kurasimisha makazi holela nchini kuanzia mwaka 2013-2023 inayolenga kurasimisha makazi mijini.

“Programu ya kitaifa ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini ya mwaka 2015-2025 inayolenga pamoja na mambo mengine kuzuia na kudhibiti ujenzi holela ambao husababisha kuwepo kwa makazi duni,” alisema.

Mbali na hilo, Mabula alisema mkakati mwingine ni kuandaa mipango kabambe ya miji kwa miji 30 kwa kushirikiana na halmashauri za miji na wilaya itakayosaidia kusimamia na kudhibiti uendelezaji wa miji.

Alibainisha hadi sasa mipango kabambe ya Arusha, Mwanza, Singida, Tabora, Mtwara, Kibaha, Musoma, Korogwe na Songea imeandaliwa na kampuni binafsi na ipo katika hatua za mwisho za maandalizi.

Alitoa mwito kwa mamlaka za serikali za mitaa kutenga fedha za kutosha katika bajeti zao kila mwaka ili kuongeza kasi ya kupima, kupanga na kumilikisha ardhi katika maeneo yao ili kuwezesha wananchi kupata makazi bora.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo