Celina Mathew
Maalim Seif |
KATIBU Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif
Hamad amefunguka kuhusu mgogoro uliokikumba chama hicho, akimtaja Profesa Ibrahim Lipumba kuwa chanzo kikuu na
kueleza jinsi asivyo na hamu hata ya kuonana naye.
Amesema kuliko kukaa meza moja na
Mwenyekiti huyo wa CUF, ni bora akatafuta viongozi wa CCM kusaka mwafaka wa
hali ya kisiasa iliyoikumba Zanzibar, “siwezi kukaa naye meza moja, yaani hata
akija hapa tulipo nitanyanyuka na kuondoka.”
Wakati Maalim Seif akisema hayo jana
katika kipindi cha 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds, Profesa Lipumba
naye alijibu mapigo baada ya kupiga simu kwenye studio za kituo hicho na
kuahidi kumjibu Maalim Seif leo kupitia kipindi hicho hicho.
Huku akijibu kila swali aliloulizwa,
Maalim Seif pia alizungumzia sababu za kutompa mkono Rais wa Zanzibar, Dk
Mohamed Ali Shein, siku ya uhuru wa vyombo vya habari, matibabu yake,
uendeshaji wa CUF baada ya kukosa ruzuku na utendaji kazi wa Rais John
Magufuli.
Alisema CCM ni maadui wakubwa wa CUF
lakini Profesa Lipumba ni adui zaidi kwa kuwa anatumika kukivuruga chama hicho.
“Ninaweza
kuzungumza na CCM kwa maana wale wanajulikana ni maadui wetu. Ukikaa nao unajua
unazungumzaje nao lakini msaliti siwezi,” alisema.
Alisema Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
alikuwa msaliti lakini aliamua kujirudi na ndiyo maana alimsamehe na hadi sasa
anafanya naye kazi.
Sumaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10
katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu, alihama CCM na kujiunga Chadema mwaka
juzi huku akigeuka mwiba mkali kwa CCM kwenye kampeni za uchaguzi mkuu Oktoba
mwaka juzi.
Maalim Seif alisema kamwe hawezi
kumsamehe Lipumba kwa maelezo kuwa ajenda yake ni kuivuruga CUF akishirikiana na
CCM.
“Lipumba ni adui mkubwa zaidi maana
kikulacho kinguoni mwako na yanayotekea sasa kwenye chama chanzo ni yeye. Kwa
sasa chama hakiwezi kutoa uamuzi wowote maana CUF kimemfungulia kesi Lipumba,
hivyop tunasubiri uamuzi wa mahakama,” alisema Maalim Seif.
“Mimi Lipumba alivyonisaliti siwezi
kumsamehe maana nina uhakika anatumika na CCM kuibomoa CUF na si kuijenga,”
alisisitiza.
Alisema endapo watashindwa kesi
mahakamani watakubaliana na uamuzi lakini watakwenda ngazi za juu.
Profesa Lipumba aliyeiongoza CUF tangu
mwaka 1995, alijiuzulu kwa hiari yake uenyekiti Agosti mwaka juzi lakini siku
chache kabla ya CUF kuitisha mkutano Agosti mwaka jana kujadili barua yake ya
kujiuzulu, aliandika barua ya kutengua kujiuzulu na akarejea kazini.
Siku ya mkutano mkuu uliofanyika Ubungo
Plaza, wajumbe waliridhia kujiuzulu kwake, lakini walipoingia kuchagua mrithi
wake, wafuasi wa Profesa Lipumba walivamia mkutano na kuuvuruga hali
iliyosababisha kusimamishwa kwake na
hatimaye kufukuzwa uanachama.
Tangu wakati huo, CUF imekuwa kwenye
mgogoro mkubwa, ikiwa ni pamoja na ofisi zake za Buguruni kutumiwa na upande wa
Lipumba, huku ruzuku za chama hicho zikitolewa kwa upande huo pekee.
Wakati hayo yakiendelea, upande wa
Maalim Sief ulifungua kesi Mahakama Kuu kupinga kurejea kwa Profesa Lipumba, kesi
ambayo washitakiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msajili wa Vyama
vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
“Siwezi kuzungumzia kugombea uchaguzi wa
mwaka 2020 wakati tuna kesi mahakamani. Nadhani suala hili tuliache mpaka Mahakama
itakapotoa haki na chama kikirudi kwenye hali ya kawaida,” alisema.
Mkono
Akizungumzia kumnyika mkono Dk Shein
walipokutana kwenye msiba wa Rais wa zamani wa Zanzibar, Alhaji Abdul Jumbe
Mwinyi, alisema alifanya makusudi, kwa maelezo kuwa Dk Shein alipora haki yake
katika uchaguzi wa Zanzibar.
“Leo wananchi wanione ninacheka naye
wataniona vipi? Nilikataa kumpa mkono kwa
makusudi ili naye akasirike na kutambua kuwa alininyima haki yangu,” alisema.
Alisema hata kodi analipa kwa shingo
upande, kwa maelezo kuwa haitambui Serikali iliyo madarakani.
Warithi
Aliifananisha CUF na timu ya mpira wa
miguu yenye wachezaji wengi, kwamba hata kama yeye atang’oka kwenye wadhifa
wake, wapo wanaoweza kuchukua nafasi.
Alitaja baadhi ya warithi wake kuwa ni Juma
Haji Duni, Mansour Yusuf Himid, Hamad Masoud, Ismail Jussa na Nassor Ahmed
Mazrui ambaye ni Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar.
Aliponda wanaodhani kuwa anang’ang’ania
kila kitu ndani ya chama hicho na kusisitiza kuwa wapo wanaomshauri ambao pia
wanaweza kuchukua nafasi yake.
“Acheni, wakati ukifika wananchi wa
Zanzibar watachomoza na kusema kwamba huyu anafaa badala ya Maalim Seif,”
alisema.
Matibabu
Akizungumzia kauli ya Rais Magufuli
aliyeshangazwa na Dk Shein kuendelea kutoa fedha za matibabu kwake wakati
alikataa kumpa mkono, alisema: “Alidanganywa na kupotoshwa. Tangu niache nafasi
ya umakamu wa kwanza wa Rais nikifanya ziara nje ya nchi najihudumia.
“Nina haki kisheria lakini kwa sababu
nawajua, nikiwaomba fedha watanipa lakini kwa kunisumbua. Najibana kwa njia
zote ili kujihudumia.”
Ruzuku
Maalim Seif pia aligusia uamuzi wa
Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, kuidhinisha ruzuku ya CUF kwa upande wa
Lipumba, kwamba kutokana na hali hiyo sasa chama kinaendeshwa kwa michango ya
wanachama.
Alisema utaratibu uliowekwa, viongozi wa
Taifa huchangia Sh 10,000, wa wilaya Sh 3,000, jimbo Sh 2,000 na mwanachama wa
kawaida huchangia Sh 1,000 kwa mwezi.
Alisema chama visiwani Zanzibar kina
wanachama zaidi ya 200,000 huku Bara wakiwa milioni 1.5.
Akumbukwe?
“Ukisema nikumbukwe kwa nini nitakujibu
nikumbukwe kwa kutunza amani, maana mimi ndiye niliomba wananchi kuwa watulivu.
Pia nimekuwa mpiganaji nisiyevunjika moyo, ninaendelea na mapambano licha ya
kuwekwa rumande miaka ya nyuma,” alisema.
Magufuli
Akizungumzia utendaji wa Rais Magufuli
tangu alipoapishwa Novemba 5 mwaka juzi, Maalim Seif alimwelezea katika sehemu
mbili; kwamba kuna maeneo amefanya vema na mengine ameharibu.
“Kuna mambo mengine yana kasoro nyingi licha
ya kuwa ni mtu anayeonekana kupigania haki, hapendi rushwa na ubadhirifu.
Tatizo lake kubwa kuna watu ndani ya Serikali yake hata wafanye nini
hawaguswi,” alisema bila kutaja watu hao.
“Huwezi kuwa kiongozi halafu vitu
vingine ukawa unaviogopa au unamwacha licha ya kuwa anafanya mambo mabaya.”
Wanahabari
Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari ambao
uliadhimishwa jana duniani kote huku nchini maadhimisho yakifanyika Mwanza,
alisema waandishi wa habari nchini hawako huru kutokana na kubanwa na sheria
kandamizi.
0 comments:
Post a Comment