Abraham Ntambara
Jaji Eusebia Munuo |
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC) kimetoa taarifa ikionesha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uhuru
wa kujieleza nchini huku ikiutaja mkoa wa Dar es Salaam kuwa kinara wa matukio
ya unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji.
Ripoti hiyo ilizinduliwa jana Dar es
Salaam na Jaji mstaafu Eusebia Munuo ambapo utafiti wa matukio hayo ulifanyika
maeneo mbalimbali nchini kati ya Januari na Desemba, mwaka jana.
Ripoti hiyo kwa mujibu wa mwandishi wake,
Paul Mikongoti imegusa masuala ya haki za binadamu, za kiraia, kisiasa, makundi
maalumu na upatikanaji huduma za kijamii.
Mikongoti, alisema mkoa wa Dar es Salaam
umeripotiwa kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji kutoka matukio 972 mwaka juzi
hadi kwa 1,030 mwaka jana.
“Kwa ujumla matukio ya unyanyasaji dhidi
ya wanawake yaliripotiwa 7,475 hadi Juni mwaka jana, jumla ya matukio hayo
17,059 yaliripotiwa mwaka juzi. Jumla ya matukio ya ubakaji 2,800 yaliripotiwa
mwaka jana, ambapo matukio hayo ya ubakaji yameongezeka kwa mwaka jana katika
mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro. Kilimanjaro yameongezeka kutoka 92 kwa
mwaka 2015 hadi 151 mwaka jana,” alisema Mikongoti.
Aidha, aliongeza kuwa kumekuwa na
matukio mengi ya nyanyaso za kingono kwa watoto nchini ambapo Dar es Salaam pia
inaongoza kwa matukio hayo.
Jumla ya matukio 345 yaliripotiwa huku Mbeya
ikifuatia kwa matukio 177 huku Morogoro
ikiwa na 160.
Alitaja sababu za kuongezeka kwa matukio
hayo kuwa ni kutokana na upelelezi wa matukio hayo yanapopelekwa kwenye vyombo
husika kufanyika taratibu, hivyo kuwa vigumu kuyathibitisha kwa mtuhumiwa wa
vitendo hivyo.
Akizungumzia haki za kiraia za kuishi
ilibainika kuwepo matukio ya kujichukulia sheria mkononi hali iliyofanya kuripotiwa
matukio 705 nchini.
Aidha, alisema adhabu ya kifo imeendelea
kutolewa ingawa tangu mwaka 1994 haijatekelezwa. Alibainisha kwamba mwaka jana watu
19 walihukumiwa ambayo ni zaidi ya watu 14 waliopewa adhabu hiyo mwaka juzi.
Mikongoti alieleza pia katika ripoti
hiyo matukio ya mauaji ya wazee na walemavu ya ngozi yaliendelea hususani mikoa
ya Kanda ya Ziwa ingawa kwa kiasi fulani hali hiyo ilipungua kutokana na elimu
ambayo imeendelea kutolewa kwa jamii.
Akizungumzia shughuli za siasa nchini
alisema haki hiyo haipo kwa kuwa tangu mwaka jana mikutano ya hadhara na
mikutano ya jinsi hiyo ilipigwa marufuku hali iliyosababisha Chadema kuitisha
maandamano ya UKUTA.
Aidha, alifafanua hali ya kujieleza
nchini ambayo ni haki ya kikatiba imeminywa kutokana na kuanzishwa kwa sheria
ya mitandao inayobana wananchi kujieleza, huku kwa upande wa vyombo vya habari
ikianzishwa sheria ya huduma za habari ya mwaka 2017 inayonyima uhuru wa vyombo
hivyo.
Jaji Munuo aliitaka Serikali kuangalia
katia masuala ya kisiasa na kuwaacha wanasiasa wafanye shughuli zao kwani ni
haki yao kikatiba huku akivitaka vyombo
vya Dola kuacha kutumia nguvu.
0 comments:
Post a Comment