Grace Gurisha
KESI ya tuhuma za uchochezi dhidi ya Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu na Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, leo inatarajia
kuendelea kusikilizwa kwa upande wa Jamhuri kutoa ushahidi kwenye Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Mbali na Lissu na Mkina washitakiwa wengine ni Jabir
Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea kusikilizwa na Hakimu
Mkazi Mkuu, Thomas Simba, ambapo upande wa mashitaka unawakilishwa na Elia
Athanas na upande wa utetezi unawakilishwa na Peter Kibatala.
Awali, aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari
Maelezo, Raphael Hokororo alidai walimpa taarifa Rais John Magufuli ya kufungwa
kwa Mawio kwa sababu jina lake lilitajwa kuwa ni mmoja wa watakaosababisha
machafuko Zanzibar.
Mkurugenzi huyo alieleza hayo wakati akijibu swali la Wakili
Kibatala, kama walimpa taarifa Rais Magufuli baada ya Wizara husika kulifungia
gazeti hilo, akajibu taarifa alipewa kwa sababu jina lake lilitajwa kwenye
habari yenye kichwa kisemacho ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Shahidi huyo alidai hatua hiyo ilifikiwa na Wizara ya
Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, baada ya wao kupeleka ripoti kuwa habari
iliyochapishwa na gazeti hilo toleo namba 182 la mwaka jana, ilikuwa na maudhui
ya uchochezi kwa walichodai ni Serikali ya Zanzibar kuongozwa na uamuzi kutoka
Tanzania Bara.
Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, mwaka jana Dar es
Salaam, washtakiwa Idrisa, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha
taarifa za
uchochezi zenye kichwa cha kisemacho, ‘Machafuko
yaja Zanzibar’.
0 comments:
Post a Comment