Grace Gurisha
Wema Sepetu |
UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kukutwa na msokoto wa
bangi inayomkabili msanii maarufu nchini, Wema Sepetu umeieleza Mahakama kuwa
upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba siku ya kumsomea maelezo ya awali.
Hayo yalielezwa jana na Wakili wa Serikali, Hellen Moshi
mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Dar es Salaam wakati kesi hiyo ilipotajwa na kuangalia kama upelelezi
umekamilika.
Baada ya Moshi kueleza hayo, Hakimu Simba aliahirisha
kesi hiyo hadi Juni mosi Wema na wenzake watakaposomewa maelezo ya awali.
Wema anatuhumiwa kukutwa na vipande viwili vya bangi
vyenye uzito wa gramu 1.08.
Mbali na Wema wengine ni wafanyakazi wake wa ndani
Angelina Msigwa (21) na Matrida Abas (16), ambao wote wanashitakiwa kwa tuhuma
moja ya kukutwa na kiasi kidogo cha dawa za kulevya.
Ilidaiwa kuwa Wema na wenzake walitenda kosa hilo
Februari 4, nyumbani kwao Kunduchi Ununio, Kinondoni, Dar es Salaam walikutwa
na misokoto hiyo.
Baada ya kusomewa mashitaka, walikana kuhusika, ambapo
Katuga alidai upelelezi wa shauri hilo haukuwa umekamilika na kuomba tarehe
nyingine ya kutajwa.
Msanii huyo na wenzake wako nje kwa dhamana ya wadhamini waliosaini
dhamana ya Sh milioni tano kila mmoja.
0 comments:
Post a Comment