Chadema yateua 6 kuwania ubunge EALA


Hussein Ndubikile

Freeman Mbowe
KAMATI Kuu ya CHADEMA imeteua wanachama wake sita kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), wakiwamo Ezekia Wenje na Lawrence Masha waliopigiwa kura za hapana katika uchaguzi uliopita.

Katika kikao kilichofanyika jana Zanzibar walioteuliwa wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu, Makamu Mwenyekiti Taifa, Profesa Abdallah Safari, Josephine Lemoyan na Pamela Massay.

Uteuzi huo ulifanyika kukiwa na kumbukumbu ya kilichotokea Aprili 4 Dodoma baada ya Masha na Wenje kushiriki uchaguzi ambao Chadema ilipeleka majina yao pekee jambo lililozua mjadala bungeni na kuhitimishwa kwa wao kupigiwa kura za hapana.

Katika uchaguzi huo, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano walichagua wajumbe saba wa EALA, sita wakiwa wa CCM na mmoja CUF.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chama hicho, Tumaini Makene ilieleza kuwa majina hayo yatakamilisha hatua zingine za uteuzi kwa mujibu wa taratibu na Kanuni za Bunge na Uchaguzi wa Bunge la EALA.

Awali, Katibu wa Bunge ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi huo, Dk Thomas Kashililah alisema uchaguzi mdogo wa kupata wawakilishi wawili wa nafasi hiyo utafanyika Mei 10.

Dk Kashililah alisema wabunge watakaopigiwa kura katika uchaguzi huo wataungana na wengine saba wa CCM na CUF.

Wabunge wa CCM waliochaguliwa ni Happiness Legiko, Maryam Ussi Yahya, Dk Abdullah Hasnu Makame, Dk Ngwaru Maghembe, Alhaji Adam Kimbisa huku kutoka Cuf akiwa ni Habib Mnyaa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo