*Asisitiza si mpya bali ya 2009 iliharibika injini
*Adai
Boeing imeiuza Tanzania kwa bei ya kuruka
Charles James
Zitto Kabwe |
KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo,
Zitto Kabwe, amesema kuna jambo Serikali inalificha juu ya ununuzi wa ndege mpya
aina ya Boeing 787-8 Dreamliner.
Akizungumza na JAMBO LEO jana,
Zitto alisema Serikali inatoa taarifa za uongo juu ya ndege hiyo, baada ya
kusema ndiyo kwanza inaundwa ilhali iliundwa tangu mwaka 2009 na kinachofanyika
sasa ni kubadilisha injini yake kwa sababu ilikuwa na matatizo ya kuwaka moto.
Mwishoni mwa mwaka jana, Rais
John Magufuli alitangaza kununuliwa kwa ndege hizo na hiyo ni baada ya kukutana
na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko wa Afrika wa Kampuni ya Boeing,
Jim Deboo kuhusu ununuzi wa ndege hiyo.
Rais Magufuli alisema ndege hiyo
ya Dreamliner 787-8 itawasili nchini Juni mwakani lengo likiwa ni kuhakikisha
Serikali inafufua shirika la ndege (ATCL) na hiyo ni baada ya kuwa tayari
imenunua ndege mbili kutoka Canada aina ya Bombadier Q400.
Akizungumzia ununuzi wa
Dreamliner 787-8, Zitto alisema hivi sasa kuna ushindani mkubwa kati ya kampuni
ya GE ya Marekani na Rolls Royce ya Uingereza, kuhusu nani apate biashara ya
kutengeneza injini hiyo mbovu.
Alisema hata ndege mbili za
Bombadier ambazo zilinunuliwa na Serikali hazikuundwa baada ya Serikali kuagiza
bali ziliundwa mwaka 2014 na tayari zilikuwa zimenunuliwa na kampuni ya ndege
ya Kazakhistan kabla ya kuuzwa Tanzania.
“Hata hizi Bombadier hazikuundwa
baada ya sisi kuagiza, bali zilikuwapo nasi tulizinunua kutoka kwa wenzetu,
ushahidi wa hili ni rahisi sana ukipanda ATCL Bombadier, tafadhali soma
maandishi madogo dirishani utaona S/N 0001519017-040 DATE 10/2014. Hiyo maana
yake ni Oktoba 2014,” alisema Zitto.
Alisema Serikali inaficha jambo
katika suala la ununuzi wa ndege hii ya Dreamliner na inajua kuwa imenunua kwa
bei kubwa kuliko ilivyostahili na hata Boeing nayo inatambua kuwa iliiuzia Tanzania
kwa bei ya kuruka huku ikiidanganya kwa kubadili injini.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa
Kigoma Mjini, alisema Serikali inajua kuwa haikusimamia maslahi ya Taifa katika
mazungumzo ya ununuzi wa ndege hizo, huku akisema ilikuwa ni bahati mbaya
mazungumzo hayo kumhusisha Rais Magufuli na Katibu Mkuu Hazina, James Doto peke
yao bila timu ya watu wanaojua kuzungumza biashara, kama ilivyo kawaida ya ununuzi
mkubwa.
Alisema Shirika la Ndege la
Boeing lilitumia uzoefu mdogo wa Tanzania na kuipiga bei kubwa na kutaka
Watanzania kutumia uhusiano wao duniani kuwataka Boeing wawajibike kwa
udanganyifu wao kwa nchi.
“Boeing wanapaswa kurudisha
sehemu ya fedha zetu, ni aibu kwa kampuni kubwa kama hiyo kuiibia nchi masikini
kama Tanzania, Watanzania mnakumbuka sakata la radar? Hii ni kurushwa zaidi ya radar.
Hela zetu zirudi tujenge reli na kuongeza ndege zingine,” alisema Zitto.
Ndege hiyo ya Boeing 787-8
Dreamliner ina uwezo wa kubeba abiria 262 na kusafiri masafa marefu bila kutua
na tayari Serikali imelipia malipo ya awali ya uundwaji wa ndege hiyo.
0 comments:
Post a Comment