Fidelis Butahe
SIKU 60 baada ya Serikali kuahidi kusaidia
waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10 mwaka huu Kagera, sasa
imebadili ‘gia angani’ baada ya kueleza kuwa misaada hiyo ni kwa ajili ya
walemavu, wajane, wagane na wagonjwa tu.
Katika ufafanuzi huo, imewataka wananchi
wengine kuanza ujenzi wa nyumba zao zilizobomoka na Serikali itasaidia pale
watakapokuwa wameishia.
Ufafanuzi huo umekuja wakati watu wa
kada mbalimbali nchini wakihoji sababu ya misaada ya mashirika, taasisi,
kampuni na watu binafsi kutumiwa na
Serikali kujenga miundombinu badala ya kusaidia waathirika wa tetemeko.
Mara kadhaa wananchi wa Kagera wamenukuliwa
wakilalamika kutopata misaada hiyo huku mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema),
Wilfred Lwakatare akitaka misaada hiyo ifikie wananchi moja kwa moja kwa
maelezo kuwa wako ambao nyumba zao zilibomoka kabisa, hawana pa kuishi.
Septemba 16 wakati akihitimisha mkutano
wa nne wa Bunge la 11 mjini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema
Serikali imetenga kodi ya miezi sita kwa kila mpangaji aliyekuwa akiishi katika
nyumba zilizobomoka kutokana na tetemeko hilo.
Alisema waliokosa kabisa hifadhi ya
makazi wamepewa mahema kwa ajili ya makazi ya muda, waathirika ambao nyumba zao
zimebomoka kabisa, wametengewa mabati 20, saruji mifuko mitano, mablanketi na
mikeka.
Lakini jana wakati akizungumza na JAMBO
LEO, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu alisema misaada
hiyo inatolewa kimakundi na wanaomulikwa ni wasiojiweza kabisa.
“Miundombinu inayojengwa ni ya hospitali
kwa ajili ya kuwatibu wao na shule kwa ajili ya watoto. Hayo ndiyo mambo
muhimu. Kuhusu kuhudumia wananchi sisi tumewagawa kwenye makundi,” alisema.
“Tunashughulikia wasiojiweza kabisa,
yaani walemavu, wajane, wagane na wagonjwa, hao ndio tumeanza nao na tayari
tumepata kundi la kwanza. Hao ndio tunawagawia saruji mifuko mitano na mabati
20.”
Kuhusu madai ya waathirika hao
kuchangiwa fedha nyingi tofauti na zile zinazotajwa, alisema: “Kuhusu zile Sh
bilioni 5, unajua majengo ya Serikali yaliyoanguka ni 1,728, ukarabati
unahitaji zaidi ya Sh bilioni 10. Pesa iliyopo sasa ni Sh bilioni 4 kwa ajili
ya kujenga hizo shule na hospitali.”
Alibainisha kuwa mifuko ya kuchangia
waathirika hao iko miwili na kwamba Sh bilioni 4 zipo katika mfuko wa Kamati ya
Maafa Kagera na kuutaja mfuko mwingine ambao una fedha zingine, zikiwamo Sh bilioni
6 zilizotolewa na Serikali ya Uingereza kuwa ni wa Kurugenzi ya Maafa Ofisi ya
Waziri Mkuu.
“Fedha zinazotoka nje zinaingia katika
mfuko huo wa Ofisi ya Waziri Mkuu, hakuna mkanganyo hapo, maana hizo fedha kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu zinaelekezwa
kwenye majengo makubwa kwa mfano shule ya sekondari Ihungo,” alisema na
kuongeza:
“Hizo Sh bilioni 6 zimetolewa kwa ajili
ya kujenga shule hiyo, ambayo ujenzi wake unahitaji Sh bilioni 22. Kiasi hicho
kilichopatikana kitajenga sehemu tu, lakini Serikali itakamilisha ujenzi. Shule
ya Nyakato nayo ujenzi wake unagharimu Sh bilioni 22.”
Alisema wananchi wa kawaida Serikali
imeagiza waanze ujenzi na itawakuta wakiendelea na itawasaidia.
“Wapo ambao tayari wameanza ujenzi, wapo
wengi tu, tutawasaidia tu maana hilo ndio jukumu la Serikali,” alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment