Mwandishi Wetu
WAKATI Rais John Magufuli akiadhimisha
mwaka mmoja madarakani, waliokuwa washindani wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka
jana wamesema licha ya mafanikio makubwa aliyoyapata rais, wananchi wake bado wanaishi
kama wafungwa.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana vyama
vinane vilisimamisha wagombea. Vyama hivyo na wagombea wake kwenye mabano ni
John Magufuli (CCM), Edward Lowassa (Chadema), Hashim Rungwe (Chauma) na
Maxmillan Lyimo (TLP).
Vyama vingine ni Anna Mghwira (ACT-
Wazalendo) Chifu Lutalosa Yemba (ADC) Fahmi Dovutwa (UPDP) na Janken Kasambala
(NRA).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanasiasa
hao walisema hakuna ubishi kwamba rais
Magufuli amefanya mambo mengi makubwa, lakini pia ni ukweli kwamba maisha ya
Watanzania hayajabadilika.
Rungwe alifananisha anachokiona sasa katika
maisha ya Watanzania na wafungwa katika nchi huru. Alisema katika kipindi hicho
cha mwaka mmoja Watanzania wamekata tamaa na hii imetokana na mfumo wa uongozi
nchini.
Alisema katika nchi za kidemokrasia
uongozi unafanya kazi na mfumo na si mtu mmoja mmoja kama inavyotaka kujitokeza
sasa.
“Mimi ninachoona katika mwaka mmoja wa
Magufuli ni Watanzania kuishi kama wafungwa, huku wakiwa hawajahukumiwa,”
alisema.
Rungwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Chauma, alisema kila kona ya nchi kuna malalamiko na lawama za hali mbaya
kiuchumi, huku njaa ikionekana kuongeza ugumu wa maisha.
“Mimi sioni jambo linafanyika kama
kipaumbele cha Watanzania, nadhani Serikali inatakiwa kubadilisha gia kwani watu
wanazidi kuwa maskini, ajira hakuna na kila kukicha ni malalamiko,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema anashangazwa kuona
Rais akifanya mambo kinyume na Katiba kwa kuzuia mikutano ya kisiasa, jambo alilosema
kuwa linaweza kuzua chuki kwa wananchi dhidi yake.
Alisema kitendo cha Rais kukataza
mikutano ya vyama siasa ni ishara tosha kuwa anaamini yeye yupo juu ya Katiba.
Mghwira alisema katika kipindi kifupi
mambo mengi yamefanyika lakini si kwa kiwango cha kuridhisha.
Alisema Rais Magufuli alipaswa kusimamia
uchumi, kupambana na rushwa, kurejesha maadili ya watumishi na kujenga umoja wa
kitaifa lakini mpaka sasa haoni mafanikio makubwa.
“Kuhusu rushwa ameanza kushughulikia
lakini anapaswa kuongeza kasi zaidi kwani hata watangulizi wake walijaribu na
wakashindwa. Jambo la msingi ni kushirikisha wataalamu katika kila ngazi na
shughuli zsa uzalishaji ziongezwe ubora,” alisema.
Mghwira alisema iwapo Rais anataka
kubadilisha nchi anapaswa kusimamia misingi ya uchumi ambayo itachochewa na
viwanda na kwamba kufikia hapo ni lazima kuwepo na maji ya uhakika na umeme.
Kuhusu umoja wa kitaifa alisema kimsingi
umetikisika na kuwa unashikiliwa na Watanzania kupenda amani, kwani kinyume na
hapo hali ingekuwa tofauti.
Alisema mtazamo wa Rais kutoruhusu
mikutano ni kinyume na Katiba na kuwa anapaswa kutambua kuwa kupitia vyama
hivyo ndio umoja wa kitaifa unakuwepo.
Mwenyekiti huyo wa ACT-Wazalendo alisema
haoni sababu ya Rais kuhofia vyama hivyo kwani vipo kikatiba na kitendo cha
kuzuia mikutano kinaweza kuleta mpasuko.
Hivi karibuni Lowassa alisema mwaka
mmoja wa Rais Magufuli umeonesha mafanikio katika baadhi ya sekta, huku sekta
ya ajira ikionekana kuwa bado ni bomu linalosubiri kulipuka.
Alisema wananchi wameonesha dhahiri
kusononeka kulingana na maisha ambayo wanaishi jambo ambalo linampa nguvu ya
kuamini kuwa anahitajika.
Lowassa alisema viongozi wana wajibu wa
kutafakari njia ambazo wanatumia kuhudumia wananchi ili kujenga msingi imara wa
maendeleo ya taifa.
“Taifa letu kwanza, mengine baadaye kwa
kuwa taifa letu ni kuu na kubwa kuliko matamanio yetu ya kuwa viongozi na
kuzidi yote taifa letu ni kuu kuzidi rangi ya bendera za vyama vyetu,” alisema.
Kwa upande wake, Dovutwa alisema anamuona
Rais Magufuli akitembea katika njia ambayo yeye alipanga kuipita iwapo
Watanzania wangemchagua.
Alisema mipango yake ilikuwa ni kuongeza
kodi, kutoa elimu bure, utumishi bora na kuboresha kilimo ambapo kwa asilimia
kubwa Magufuli ametekeleza.
Hata hivyo, Dovutwa alisema Rais
anapaswa kuongeza nguvu katika kilimo ili kuhakikisha dhamira yake ya kujenga
viwanda inafakiwa wakati ukifika.
“Siwezi kusema kuwa amepatia kwa
asilimia 100 ila kimsingi maeneo mengi amenigusa naamini akipewa muda
atafanikisha mtazamo wake wa kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati.
Lyimo naye alisema anaona mwelekeo mzuri
wa uongozi kwa Rais Magufuli na kuwa suala la uchumi litakaa vizuri siku za
karibuni.
Lyimo alisema Rais Magufuli ameonesha
jitihada za kunyoosha nchi ambayo ilikuwa imepoteza muelekeo hivyo anapaswa
kuungwa mkono na wananchi wote.
Aidha, Lyimo alisema katika kuminya
demokrasia hawezi kuungana naye kwani anavunja Katiba na kumshauri kufanya
aliyoyaahidi kwa wananchi ili wapinzani wakose la kusema baadaye.
0 comments:
Post a Comment