Salum Maige, Geita
JAMII za
wakulima na wafugaji zilizovamia Hifadhi ya Taifa ya Misitu ya Geita mkoani
Geita, zimeingia kwenye mgogoro baada ya wafugaji kuwatuhumu wakulima kujeruhi
ng’ombe zao kwa mapanga.
Mgogoro huo pia
unadaiwa kutokana na wakulima kuvamia vyanzo vya maji na kuendesha shughulisha
za kilimo, huku wafugaji wakitumia vyanzo hivyo kunywesha mifugo yao na kulisha
ngombe zao.
Baadhi ya
wafugaji walisema kwa nyakati tofauti kuwa matukio ya ng’ome kukatwa mapanga
yameanza kutokea tangu mwaka jana na hadi sasa tayari ng’ombe wanane
wamejeruhiwa.
“Juzi saa 10
jioni alikamatwa mfugaji Robert Kabulizina na wakulima kwa kushirikiana na
mgambo akapelekwa hadi kituo cha polisi akituhumiwa kulisha mifugo kwenye mazao
ya Bahati yaliyo kwenye hifadhi hiyo. Kwa kuwa tatizo hilo limekuwa kwa muda
mredu, tunaiomba Serikali iingilie kati kulitatua kwani yanaweza kutokea
mauaji,”alisema mfugaji Mapinduzi Salehe.
Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Geita, Modest Apolinary, Ofisa Mazingira Pancrace
Shwettelele pamoja na Mwenyekiti wa Mtaa wa Upendo ulio jirani na hifadhi hiyo,
Dk Deodratias Katunzi juzi walitembelea maeneo yenye mgogoro huo kujionea hali
halisi.
Dk Katunzi alimwambia
mkurugenzi huyo kuwa kwa sababu wote wakulima na wafugaji wana makosa ya
kuvamia hifadhi, Serikali inapaswa kuangalia utaratibu wa kuwasaidia wafugaji
kupata maeneo ya kuchungia na kunyweshea mifugo wao.
“Wafugaji hawana
maeneo kabisa ya kufugia mheshimiwa mkurugenzi, lakini wakulima wana maeneo ya
kulima, kinachotakiwa ni Serikali kuangalia utaratibu wa kutenga maeneo ya
kuchungia mifugo,”alisema Dk Katunzi.
Hata hivyo, mkulima
Deus Kulwa alisema kinachowafanya wavamie hifadhi hiyo na kujishughulisha na
kilimo ni umasikini unaowakabili na kwamba wamekuwa wakijishughulisha na kilimo
cha mazao ya chakula na biashara kwa ajili ya kujipatia kipato.
Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Geita, aliunda timu ya watu 12 ya wakulima na wafugaji yenye
kazi ya kuhakikisha hakutokei tena uharibifu wa mazingira ndani ya hifadhi
hiyo.
0 comments:
Post a Comment