* Hakuna mwenye maono ya Nyerere, wala wa kufuatwa
* Asikitishwa na ‘panya road’ asema ni mfano wa maadili
Suleiman Msuya
“TAIFA
limepoteza mwelekeo. Balaa ambalo tumepata miaka 17 ya kutokuwepo Mwalimu Nyerere
tunapaswa kufakari ili turejeshe taifa kwenye reli yake,"
Hivyo ndivyo
alivyosema Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi jana katika Kongamano
la Kumbukumbu ya miaka 17 ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere
lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Nyerere
alifariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, Uingereza
alipokuwa akitibiwa saratani ya damu na kuzikwa kijijini kwake Butiama mkoani
Mara.
Katika kongamano
hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi, Mwinyi alisema Taifa linapaswa
kujadili ni wapi watu wake wamekosea na sababu yake ili kuweza kumuenzi
Nyerere.
“Tangu Nyerere alipofariki
dunia, Taifa limekuwa na mmomonyoko wa maadili, huku ikionekana dhahiri kuwa
hakuna wa Mtanzania mwingine wa kufuatwa,” alisema Mwinyi.
Rais mstaafu huyo
alisema ni jambo la kusikitisha kuona kunakuwapo kundi linaloitwa 'Panya roads'
huku kukiwa hakuna hatua za kueleza sababu na kukukabiliana nalo.
"Nadiriki
kusema Taifa limepoteza mwelekeo na mbaya zaidi kuna kila dalili kuwa hakuna
mwenye maono ya Nyerere kurejesha maisha yake kwa jamii yetu," alisema
Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa.
Alisema kwamba hayati
Baba wa Taifa alikuwa zaidi ya kiongozi, hali ambayo ilimwezesha yeye (Mwinyi)
kufikia alipofikia lakini kwa siku za karibu kumekuwa na uvunjifu wa maadili
katika uongozi.
Mwinyi alisema
ni jukumu la kurejea katika mafundisho ya Mwalimu ili kuweza kurejesha heshima
ya nchi ambayo kwa sasa imekosa wakuigwa.
Alisema malalamiko
ambayo yanaendelea katika jamii leo ni ishara tosha kuwa tunapaswa kujitafakari
kama Taifa linalotaka kumuenzi Nyerere.
Mwinyi alisema
kinachoonekana ni kama gari limekatika usukani hivyo makongamano ya Kumbukumbu
ya Nyerere litumike kutafakari hatma ya Taifa.
Alisema Nyerere
aliondoka akaacha nchi ikiwa maskini na hadi sasa haijawa tajiri ila wapo
matajiri wachache ambao wanaendelea kuleta mpasuko.
Alisema
Nyerere aliamini katika ukweli, uadilifu ambao ulichangia ukombozi
na kujiamini ila leo imefikia kuzalisha hadi panya roads ambao zamani
hawakuwepo.
Rais Mwinyi
alisema katika ulimwengu wa sasa askari wanaogopwa na kukimbiwa hivyo ni jukumu
la jamii kujiiza nini sababu.
Aidha, Mwinyi
alihoji nini sababu ya udini kushika kasi kwa siku za karibuni na kwamba
utaratibu huo haupaswi kuwa msingi wa maisha ya Mtanzania .
Rais mstaafu
Mwinyi alisema leo imefikia watu wanaogopa kutaja majina ya ukoo wakihofia
kukosa kazi jambo ambalo halikuwepo kwa utawala wa Nyerere.
"Tusikubali
kuliacha taifa kama kishada kilichokatika uzi, inakuwaje nchi
inakuwa kama haina mwenyewe, hakuna mwenye sauti Mwalimu
hakutuacha hivi, " alisema.
Kwa upande wake
Profesa Issa Shivji alisema katika kumuenzi Mwalimu watanzania wanapaswa
kuangalia mambo matatu ambayo ni falsafa yake, msingi wa umoja wa kitaifa na
azimio la uongozi.
Alisema kupitia
misingi hiyo Nyerere aliweza kuishi na makundi yote bila tatizo jambo ambalo
kwa sasa halipo.
"Uongozi ni
njia ambayo inahitaji ushikiano na si kufikiria utawala huwezi kufika hasa
katika kizazi hiki cha kuhoji, " alisema.
Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS),
Dk. Hans Kitine alisema katika miaka 17 ya kutokuwepo kwa Nyerere Taifa
limegubikwa na rushwa ya hali ya juu hali inayosikitisha.
Kitine alitoa rai kwa washauri wa Rais John Magufuli
kumshauri kuhusu uongozi pamoja na kutambua kuwa Rais ni taasisi na si mtu
mmoja.
“Mimi siogopi kusema hili pamoja na kuwa halikuwa katika
ajenda naomba washauri wa Rais wamshauri kuwa Rais ni taasisi si mtu binafsi na
nikipata nafasi nitaenda kumueleza,” alisema Kitine.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyehudhuria
kongamano hilo alisema: “Jitihada alizofanya Mwalimu katika kujenga demokrasia
zilisimamia hoja, lakini kwa sasa ukiwa na hoja unapata misukosuko. Mfano leo
hii, Rais amezuia watu kwenda kwenye sherehe za kuzima Mwenge, Hivi
ameshirikisha nani wakati fedha hizo zilipitishwa bungeni?”
Msaidizi wa mwisho wa Nyerere, Samweli Kasoli alisema
ujumbe alioachiwa na Baba wa Taifa ni Watanzania kutomlilia yeye bali walilie
Tanzania yao.
0 comments:
Post a Comment