Viongozi wadaiwa kuuza ardhi ya viwanda


Sharifa Marira

Mohamed Mchengerwa
WAKATI Serikali ikijinadi kuwa ya viwanda, watendaji wake wamekwenda kinyume kwa kuuza eneo lililotengwa kwa ajili ya viwanda wilayani Rufiji, Pwani ekari moja Sh 10,000.

Taarifa ya kuuzwa kwa eneo hilo ilitolewa na wananchi wa kijiji cha Chumbi wilayani humo kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge Mohamed Mchengerwa kwa lengo la kushukuru kwa kumchagua na kusikiliza kero zao.

Katika Mkutano huo juzi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa  CCM wa Wilaya, Mussa Mngeresa alieleza kuwa eneo hilo lililokuwa na ekari zaidi ya 2,400 liliuzwa  kwa Sh milioni 24 hivyo kila moja   kwa Sh 10,000 bila wananchi kushirikishwa.

"Uuzwaji huu ulifanywa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Chumbi C ambaye pia ni Diwani wa Chumbi, Salum Mtimbuko (CCM)  na alipata baraka za Mkuu wa Wilaya, Juma Njwayo, ambaye wananchi walimweleza suala hilo kabla, lakini hakulifanyia kazi na kuwataka waache alichokiita ni majungu,’’ alisema.

Alisema viongozi hao waliudhi wananchi kwa kuuza ardhi kwa mwekezaji ambaye wanamjua na kwamba ukifanyika uchaguzi wakati wowote kabla masuala hayo hayajatafutiwa ufumbuzi, CCM itapoteza nafasi, hivyo kumwomba Mbunge kufanya jitihada za kuleta viongozi wa mkoa, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Akizungumzia suala hilo, Mchengerwa alilaani kitendo cha viongozi hao kutaka kukwamisha maendeleo ya viwanda jimboni kwani alishazungumza na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kuhusu ujenzi wa kiwanda cha sukari katika eneo hilo.

“Jamani huku ni kurudishana nyuma na kutotambua juhudi za Serikali na tunaowatetea, haiwezekani viongozi wahusike kuuza ardhi ya kiwanda, wananchi tusikubali, sheria inaruhusu kuongea upya na mwekezaji huyo, ili atuachie ardhi yetu au aongeze fedha tukatafute eneo lingine, kuuza Sh 10,000 ekari moja ni aibu,’’ alisema.

Akijibu tuhuma hizo Diwani Mtimbuka alisema: “Nyie mnanionea wivu, wengine nimewasadia sana kuwalisha na familia zenu, au kwa sababu mnaniona naishi vizuri na wake zangu wawili na nina nyumba na magari? Pumbavu.’’

Majibu ya Diwani yalizua tafrani kwa wananchi kumzomea na kumtaka Mchengerwa arudi siku nyingine na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, ili atatue kero zilizopo, kwani viongozi wanauza maeneo kiholela na wanaposhitaki kwa Mkuu wa Wilaya, anakuwa upande wa wauzaji.

Mchengerwa aliwaeleza wananchi hao kwamba ameshawasiliana na Ndikilo na kuahidi kufanya ziara maeneo hayo Desemba 5.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo