Makamba asikitishwa na mazingira


Suleiman Msuya

January Makamba
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba, amesema anasikitishwa na uharibifu wa mazingira nchini aliouelezea kuwa ni kizingiti cha maendeleo ya nchi.

Aidha, Makamba amesema Serikali iko kwenye mchakato wa kutangaza maeneo nyeti ya mazingira katika mikoa ya Mbeya na Rukwa, ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Makamba alisema hayo jana wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari nchini kuhusu ziara aliyofanya kwenye mikoa tisa nchini.

Alisema jitihada za Serikali kukabiliana na changamoto za umasikini na kukuza uchumi, zitafikiwa iwapo jamii itabadilika na kutunza mazingira kwa kushirikiana na wadau.

Makamba alisema katika ziara aliyofanya kwenye mikoa ya Morogoro, Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma na Tabora, alibaini uharibifu mkubwa wa mazingira, hali ambayo inaweza kusababisha janga kwa nchi.

Alisema Rukwa uharibifu mkubwa umefanyika kwenye Ziwa Rukwa hali ambayo imesababisha viboko kuathirika zaidi.

Makamba alisema kwenye Mto Katuma ambao ndio mhimili wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi, walihesabu michepuko 40 ambayo imesababisha maji yasifike mbugani na hivyo kusababisha viboko na wanyama wengine kutaabika na hata kufa.

Aidha, katika uharibifu wa misitu alisema takwimu zinaonesha zaidi ya heka 1,000 zinakatwa miti kila siku ambapo kwa mwaka zaidi heka 367, 000 zimekatwa.

"Hali ya uharibifu wa mazingira ni mbaya, wapo watu wanakata hadi mininga kwa ajili ya kukausha tumbaku, nadhani ni wakati wa kuamka kukabiliana na hali hii," alisema.

Makamba alisema wakataji miti wanaingia katikati ya misitu na kukata, hali ambayo inasababisha wasimamizi kutotambua haraka.

Alisema uharibifu upo pia kwenye uchimbaji madini ambapo baadhi ya wachimbaji wamekuwa wakitumia sumu na kuathiri mazingira, wananchi na wanyama.

Alibainisha kuwa ng'ombe ni tatizo kubwa katika uharibifu wa mazingira na kwamba wako kwenye mchakato wa kushirikisha wadau na wizara zingine, ili kufikia mwafaka.

Alisema katika kukabiliana na hali hiyo, wameelekeza milima ya Mbeya na Mto Rukwa kuwa maeneo nyeti ya mazingira, ambapo Serikali itatangaza kwenye Gazeti la Serikali mapema mwakani.

Makamba alisema awali Mlima Mbeya ulikuwa na vyanzo 50 vya maji, lakini kutokana na uharibifu wa mazingira vimebakia vinne ambavyo ni vichache, jambo ambalo litachangia ukosefu wa maji kwa siku za karibuni, kama hakuna hatua zitachukuliwa.

Alisema ameagiza kuandikwa sheria ndogo za kusimamia mazingira vijijini, kuundwa kwa kamati, kufanyika tathmini za athari za mazingira na kuitishwa kikao kikubwa cha wadau ili kujadili hali ya mazingira.

Waziri alisema ameelekeza Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lihakikishe ndani ya mwaka mmoja, liwezeshe wakimbizi kuacha kukata miti kwa ajili ya kuni na kufanya tathmini ya athari ya mazingira.

Hali kadhalika alisema wameyapa maeneo sita kipaumbele ili kukabiliana na hali hiyo ambayo ni uwepo wa NEMC, Ofisi ya Makamu wa Rais na Halmashauri kujengewa uwezo, kupunguza matumizi ya mkaa na kuimarisha uwezo wa taasisi.

Maeneo mengine ni kutafuta rasilimali, kuweka msukumo mpya kwenye upandaji wa miti nchini na kuondoa matumizi ya mifuko ya plastiki.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo