Serikali yatoa onyo kali kwa Mtanzania


Mary Mtuka

Dk Jakaya Kikwete
SERIKALI imetoa onyo kali kwa Gazeti la Mtanzania kwa ilichoeleza kuwa ni gazeti hilo kuandika habari zisizo za kweli na zilizolenga kumdhalilisha Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Mbali na onyo hilo kwa Mtanzania, Serikali imesema haitasita kuvichukulia hatua kali za kisheria vyombo vya habari vitakavyokiuka maadili na itaendelea kuheshimu uhuru wa vyombo hivyo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana iliyosainiwa na Kaimu Msajili wa Magazeti, Patrick Kipangula, Serikali ilisema Mtanzania toleo namba 8370 ya Novemba 20 na toleo 8372 la Novemba 22, ilichapisha habari zenye vichwa vya habari,'JK azuiwa Uwanja wa Ndege' na Ukweli Safari ya JK Uarabuni' zikieleza kukwama kwa msafara wake kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimatafa wa Mwalimu Julius Nyerere.

"Habari hizo si za kweli na zililenga kumdhalilisha Rais mstaafu na familia yake, Serikali imesikitishwa na jambo hilo, kwani zilipotosha umma wa Watanzania na kuacha wakijiuliza maswali," alisema Kipangula na kuongeza:

“Kupitia uzito wa tuhuma za gazeti hilo kwa kiongozi huyo mstaafu tunatoa onyo kali na endapo kitendo hicho kitajirudia tena, basi hatua kali zitachukuliwa.”

Taarifa hiyo ilivikumbusha vyombo vya habari kuzingatia maadili ya tasnia ya habari badala ya kuandika na kutangaza habari zenye lengo la kutaka kugombanisha viongozi wastaafu na Serikali iliyoko madarakani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo