Mashaka Mgeta
Mashaka Mgeta |
MWISHONI mwa wiki iliyopita, Jumuiko la Maliasili
Tanzania kupitia kampeni ya Mama Misitu, iliwakutanisha wahariri na waandishi
waandamizi katika semina na ziara iliyowafikisha kwenye maeneo yenye msitu wa
Ruvu Kusini mkoani Pwani.
Ni mafunzo yaliyoibua hitaji la ‘nguvu zaidi’ katika
kuchagiza kasi ya vyombo na waandishi wa habari kuelimisha, kutetea na kutoa
taarifa zinazohusiana hifadhi ya misitu.
Takwimu zinazotokana na tathmini ya rasilimali za misitu
iliyofanyika mwaka 2013, zinaonesha kuwa tani milioni moja za mkaa kila mwaka
hutokana na ukataji wa misitu iliyopo kwenye eneo linalokadiriwa kuwa na ukubwa
wa hekta milioni 48.1 nchi nzima.
Pia utafiti uliofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu
(TFS) ulionesha kuwa katika uhifadhi, Tanzania inapoteza hekta 400,000 za
misitu kila mwaka kupitia matumizi ya kuni, mkaa, mbao, ujenzi na uchomaji moto
misitu.
Zipo athari nyingi zinazotokana na uharibifu wa misitu
kiasi kwamba hata zikiorodheshwa na kufafanua hapa, nafasi iliyopo kwenye safu
hii haitatosha.
Lakini misitu ikiwa ni sehemu ya ‘maumbo’ ya mazingira
yanayohitaji kutunzwa, ina manufaa lukuki katika maisha ya binadamu na mimea.
Misitu ni makazi, hifadhi ya vyanzo vya maji, `kivutio’ cha mvua kunyesha,
hifadhi ya rasilimali kama madini na mahali ambapo shughuli za kibinadamu
zinafanyika.
Ndio maana ziara iliyowafikisha wahariri na waandishi wa
habari waandamizi kwenye msitu wa Ruvu Kusini, haikuwa mfano wa utalii wa
ndani, bali ni kupata ukweli wa namna msitu huo, miongoni mwa mwingine,
unavyohifadhiwa, kunufaisha jamii zinazoishi kuuzunguka, changamoto zilizopo na
namna bora ya kuzitatua.
Kwa bahati nzuri, wakazi wa vijiji 11 vya wilaya za Kibaha
na Kisarawe vinavyouzunguka msitu wa Ruvu Kusini wamenufaika kupitia mafunzo
yaliyotolewa na waelimishaji wa kampeni ya Mama Misitu, hivyo kuwa na uelewa
mpana wa masuala yanayohusu sheria, kanuni na sheria ndogo, miongoni mwa mambo
muhimu ya ushiriki wao katika uhifadhi wa msitu huo.
Meneja wa Msitu wa Ruvu Kusini wa TFS wenye ukubwa wa
hekta 30,633, Nassoro Mzava, anavitaja vijiji hivyo kuwa ni Soga, Boko Mnemela,
Kibomwendwa, Malangalanga, Mtamba, Kifuru, Mpiji, Chakuge, Kisanga Kona, Sangwi
na Kipange.
Latifa Felex, ni mjumbe wa kamati ya ardhi na mazingira
ya kijiji cha Soga, anasema kabla ya kupata mafunzo kupitia Mama Misitu, jamii
zinazoishi kuuzunguka msitu huo hazikutambua manufaa yam situ, badala yake
zikawa sehemu ya matukio yaliyochangia uharibifu wake.
Anasema ulinzi na uhafadhi wa msitu wa Ruvu Kusini
ilikuwa ni miongoni mwa mambo yaliyofikiriwa kuwa kati ya majukumu ya Serikali
kupitia vyombo vya ulinzi na usalama. “Lakini baada ya kupata kuwezeshwa
kupitia mafunzo ya Mama Misitu na wadau wengine ikiwamo Serikali, tumetambua
wajibu wetu na sasa tunashiriki katika ulinzi na uhafadhi wa msitu,” anasema.
Hata hivyo, mchakato wa kuwapo ushiriki timilifu bado
haujafikia kilele chake kutokana na changamoto kadhaa ikiwamo ya kutokuwapo kwa
mpango wa usimamizi uliopitishwa na kutosainiwa kwa mikataba ya makubaliano
kati ya TFS na vijiji vinavyozunguka msitu wa Ruvu Kusini.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kipangige, Shomari Juma anasema
kukosekana kwa ushirikiano madhubuti kati ya wananchi na TFS kunazorotesha
ufanisi katika maeneo tofauti yenye tija, miongoni mwa hayo ikiwa ni uwasilishaji
wa tozo zinazotokana na mazao ya misitu kwa vijiji husika.
“Hivi sasa hakuna mfumo rasmi unaotambulika kupitia
makubaliano ambayo bado hayajasainiwa, hivyo marejesho yanayofanyika sasa
yanategemea zaidi utashi wa TFS, hali ninayodhani inaweza kufifisha ari ya
wanajamii kushiriki ulinzi na uhifadhi wa msitu huo,” anasema.
Lakini Mzava anasema ingawa changamoto hiyo (iliyotajwa)
ipo, mfumo wa makusanyo na matumizi ya fedha za umma kupitia TFS inasababisha
mchakato wa kurejesha fedha vijijini kuchukua muda mrefu, hali inayoweza
kufifisha ari ya ushiriki wa wananchi kuhifadhi na kuulinda msitu huo.
Anafafanua kwamba fedha zinazohusika katika ‘eneo’ hilo
ni zinazotokana na faini zinazotozwa kwa watu wanaokutwa wakiharibu misitu na
ambazo kiasi chake kinatozwa kutokana na tofauti za mazingira na sababu zilizoainishwa
kwenye sheria, kanuni na miongozo inayohusiana na misitu.
kukwama kwa makubaliano ama mikataba kati ya TFS na
vijiji vinavyouzunguka msitu wa Ruvu Kusini, kunachangiwa pia na vijiji husika
kushindwa kufanya mikutano ya kijiji ili kuwapa fursa wananchi kujadili na kupitisha
maazimio yanayohusiana na mikataba husika.
Kwa mujibu wa Mzava, kiasi cha vijiji vitano kati ya 11
vilivyopo, vimefanikisha kuitisha mikutano hiyo na kupitisha makubaliano ya
ushirikiano na kwamba vijiji vilivyobaki havijafikia hatua hiyo.
Pia Mzava anasema licha ya hali hiyo, TFS inaendelea
kushirikiana na kamati za ardhi na mazingira za vijiji vyote kufanya doria kwa
kadri inavyohitajika, ingawa katika mazingira na nyakati kadhaa, wajumbe hao
hawashirikishwi hasa katika kupanga ratiba ya siku ya doria.
“Imetokea mara kadhaa kwamba wajumbe wa kamati hizo
wanapojulishwa kuhusu siku na wakati wa doria, wanazipenyeza taarifa hizo kwa
wahusika na hivyo kuwapa mwanya wa kuikwepa doria,” anasema.
Afisa Mwandamizi wa TSF, Makao Makuu jijini Dar es
Salaam, Emmanuel Msofe, anasema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kutathmini
na kuchunguza mazingira misitu ili kuchapisha ama kutangaza habari zenye tija
na ufanisi unalenga katika uhifadhi na ulinzi wa rasilimali hiyo.
Msofe anasema hatua hiyo itafikiwa waandishi wa habari
watapata uelewa mpana, uzoefu na ushiriki katika masuala yanayohusu misitu, ili
kuzifanya habari zao kuwa zenye kuleta mijadala na mabadiliko chanya.
Msofe anaeleza namna misitu inavyotegemewa katika uhai wa
viumbe na shughuli za binadamu na kwamba hivi sasa Serikali kupitia Wizara ya
Maliasili na Utalii inazipitia ili kufanya maboresho kwenye Sheria ya Misitu ya
mwaka 1998, hali itakayotokea pia kwenye kanuni zake.
0 comments:
Post a Comment