Mwandishi Wetu
Zitto Kabwe |
KIONGOZI wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameitaka Serikali
itangaze rasmi baa la njaa kwa mujibu wa sheria, kwa maelezo kuwa hali si nzuri
na gharama za maisha zinazidi kupanda.
Zitto alitoa kauli hiyo jana wakati akimnadi mgombea
udiwani wa kata ya Nkome, Geita ambapo alisema akiwa kwenye ziara Morogoro
alizungumzia hali hiyo kwa nchi nzima.
"Hali ya chakula nchini si nzuri. Wananchi
mmeshuhudia namna bei za vyakula zinavyopanda kila siku. Bei ya sembe sasa kilo
moja imefikia Sh 1,600 Morogoro. Mchele kilo Sh 1,500, maana yake leo ugali na
wali bei inafanana. Gharama za maisha zitaendelea kupanda kutokana na uhaba wa
chakula kuwa mkubwa,” alisema.
Alisema hali hiyo inatokana na uamuzi mabovu ya Serikali katika
hifadhi ya chakula na tofauti na viongozi waliopita, ambao walikuwa wakinunua
chakula cha akiba ili wakati wa ukame chakula hicho kiingie sokoni.
"Hivyo kushusha bei na kuwezesha wananchi kumudu
gharama za chakula. Rais wetu kawaambia wananchi wa Kagera kwamba Serikali
haina shamba, hivyo hakuna chakula cha njaa. Hii kauli si ya uongozi. Ni kauli
ya kuficha uamuzi wa Serikali yaliyotusababisha kukosa akiba ya chakula," alisema.
Alinukuu zaidi kwamba ghala la chakula la Taifa lina tani
90,000 tu za chakula. Kipindi kama hiki mwaka juzi ghala la chakula lilikuwa na
tani 450,000. Chakula kilichopo kwenye ghala kinatosha kwa wiki moja tu.
Takwimu hizi zote zipo kwenye taarifa ya Benki Kuu ya Mapitio ya uchumi ya Novemba.
Alisema alishangazwa na hatua ya Waziri wa Kilimo, Mifugo
na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alijibu hoja hizi kwa wepesi na kusema Tanzania ina
chakula cha kutosha pia alipoulizwa kuhusu kiasi kilicho kwenye Ghala la Taifa
( NFRA ), alijibu kwamba hawezi kutaja kwa sababu za kiusalama..
Hata hivyo, alisema takwimu za kiasi cha chakula zipo
kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na hivyo kutaka kujua hizo ni
taarifa za wapi. “Ni dhahiri Waziri wa Kilimo alikuwa anajaribu kuficha kwa kuogopa
kutumbuliwa kwa kusema hali halisi ya chakula nchini,” alisema Zitto.
Alimpongeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kuamua kutembelea
NFRA na kujionea hali halisi.
“Huu ndio uongozi, badala kukanusha habari ambazo ni za kweli
na kuthibitishwa na taasisi za Serikali kama BoT. Waziri Mkuu anapaswa kuchukua
hatua dhidi ya viongozi wa Serikali wanaoficha ukweli kuhusu baa la njaa
nchini.
"Waziri anasema kama wananchi wanaona ugali ni aghali
wale wali. Anasema kuna mchele mwingi nchini lakini umeshikwa na watu binafsi.
Waziri anataka kuwaambia Watanzania kuwa hivi sasa Serikali inategemea chakula
cha watu binafsi ambao haijui idadi ya tani zilizopo kushughulika na suala la
njaa. Hii ni ajabu kubwa sana,” alisema.
Alimshauri Waziri Mkuu achukue hatua muhimu za kisheria
kutangaza baa la njaa nchini kwa kuwa tamko hilo litaisaidia kupata bajeti ya
dharura ya kununua chakula na kutoa uhuru kwa wakuu wa wilaya kutangaza bila
woga kuwa maeneo yao yana njaa na bila kufanya hivyo, italeta maafa makubwa kwa
sababu wakuu wengi wataendelea kuficha njaa.
0 comments:
Post a Comment