Edith Msuya
Johnson Minja |
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania,
Johnson Minja, amesema wataendelea kufunga biashara, kama maeneo ya
wafanyabiashara hayataboreshwa ili kuwavutia.
Minja alisema hayo jana kwenye mahojiano maalumu na kituo
kimoja cha redio, kuhusu kufungwa kwa biashara Dar es Salaam.
Alisema awali wakati Serikali inaingia madarakani,
ilijipambanua kuwa itahakikisha watu wanalipa kodi, ili kukuza uchumi wa nchi.
Minja alisema walikubali mpango huo wa Serikali kutokana
na malengo yake mazuri kwa wafanyabiashara ya kuleta ushindani kwenye biashara.
"Baada ya hapo, kuliibuka mfumuko wa kodi bandarini
kutokana na mahesabu ya upitishaji mizigo,” alisema.
Alifafanua kuwa hakukuwa na kodi mpya, bali kilichofanyika
ni kwa wenye mzigo bandarini kuongezwa thamani ambapo mwenye mzigo wa Sh milioni
30, alijikuta ukibambikiwa Sh milioni 200.
"Na hii si kodi mpya, bali ni yale mahesabu ya
ushuru wa forodha," alisema na kuongeza kuwa baada ya kubaini hilo, walitembelea
nchi mbalimbali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutafuta
mbinu za kudhibiti ubambikiwaji wa thamani za mizigo.
Alitaja nchi walizotembelea kuwa ni Kenya na Uganda,
ambako walikuta kodi zikikatwa kulingana na thamani halisi ya mzigo na hakukuwa
na ubambikizaji.
Minja alisema kama uchumi wa nchi unakua, anaiomba
Serikali ihakikishe ukuaji huo unamgusa mwananchi wa kawaida, ili kuondokana na
malalamiko.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya uchumi
kwa mwishoni mwa mwaka jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango
alisema pamoja na uchumi kukua kwa asilimia 7.2, baadhi ya wafanyabiashara
walifunga karibu maduka 2,000.
Kwa mujibu wa Dk Mpango, utafiti uliofanyika Dar es
Salaam na Arusha kati ya Agosti na Oktoba mwaka jana, ilibainika katika wilaya
ya Ilala wafanyabiashara wakifunga maduka 1,076.
Dk Mpango alisema kwa Kinondoni biashara 443 zilifungwa
na kufuatiwa na Temeke, ambako biashara 222 zilifungwa huku Arusha,
wafanyabiashara 131 wakifunga biashara zao.
Alitaja aina ya biashara zilizofungwa kwa wingi kuwa ni
za sekta ya ujenzi na biashara ya jumla na rejareja na chache zikiwa kwenye
huduma za usafiri.
0 comments:
Post a Comment