*Watozwa 30,000/- kwa kila kosa tofauti na utaratibu
*Mpinga
asema taarifa yake inakanganya aahidi mpya
Mwandishi
Wetu
WAKATI Jeshi la Polisi Kikosi cha
Usalama Barabarani likiendelea na operesheni zake, ikiwamo ya kukamata madereva
wa magari na pikipiki wanaovunja sheria na kuwatoza faini za papo kwa hapo, imebainika
kuwapo dhuluma katika faini hizo.
Jana kupitia mitandao ya kijamii, Jeshi
hilo lilianisha makosa ya barabarani yapatayo 20 na adhabu zao ikiwa ni faini
na vifungo jela, huku katika baadhi ya makosa, faini zilizoainishwa
zikitofautiana na zinazotozwa barabarani.
Adhabu zilizoanishwa ni faini za kati ya
Sh 10,000 hadi Sh 50,000 na kifungo cha kati ya miezi sita hadi miaka miwili au
vyote kwa pamoja kwa kosa.
Hata hivyo, mbali ya adhabu hizo
kuanishwa kwa makosa ya barabarani, askari wa barabarani wamekuwa wakitoza
faini isiyopungua Sh 30,000 madereva kwa makosa hata yasiyostahili kutozwa, na
hivyo kuzua maswali mengi.
Licha ya hali hiyo, Kamanda wa Kikosi
cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga aliyezungumza jana na JAMBO LEO alikiri viwango
vya adhabu hizo kutolewa, lakini akasema taarifa hiyo inakanganya wananchi akisema
wanatoa tafsiri tofauti huku akieleza kwamba, wapo katika mchakato wa kutoa mchanganuo
mwingine.
“Hizi ni adhabu za mahakamani, endapo
mtu atapelekwa mahakamani, ndiyo maana utaona na vifungu vimeainishwa lakini
kwa makosa ya papo kwa hapo ni Sh 30,000 kwa kosa,” alisema.
Baadhi ya madereva waliozungumza na
gazeti hili walishangazwa na viwango vya faini wanavyotozwa barabarani wakati
sheria ikiweka wazi adhabu husika.
“Mfano ukisahau leseni sheria inataka
ulipe faini ya Sh 10,000 lakini tunatozwa Sh 30,000, hii si dhuluma? Naona
madereva tunadhulumiwa,” alisema Shabani Ally dereva wa daladala la Buguruni-Chanika.
Joel Ndundu dereva wa bodaboda, Upanga
alisema: “Faini tunazotozwa hazilingani na uhalisia bali trafiki hujiamulia,
sijui wanapata asilimia 10?”
Makosa
20
Katika mchanganuo huo, mtu akiendesha
gari amelewa au kuathiriwa na dawa za kulevya kwa zaidi ya kiwango cha asilimia
0.80 adhabu yake ni faini ya kati ya Sh 15,000 na Sh 50,000 huku adhabu
nyingine zikiwa ni kifungo kati ya miaka miwili hadi mitano jela.
Kosa la kutofuata alama za barabarani,
ikiwa ni pamoja na taa za barabarani na sehemu wanayovuka waenda kwa miguu,
faini ni kati ya Sh 15,000 hadi Sh 30,000 au kifungo cha miezi sita jela au
vyote pamoja.
Kuendesha gari kwa kasi isiyoruhusiwa
katika eneo husika, adhabu ni faini ya Sh 15,000 hadi Sh 50,000 au kifungo cha miaka
miwili na kisichozidi mitano.
Inafafanua kuwa dereva akisahau leseni ya
udereva, faini ni Sh 15,000 au kifungo cha miezi sita au vyote pamoja, kutojua
leseni iliko faini ni Sh 20,000 hadi Sh 50,000
au kifungo cha miezi sita jela au vyote.
Kosa la kutumia leseni iliyokwisha muda
wake, faini ni Sh 15,000 hadi Sh 30,000 au kwenda jela miezi sita, kutokuwa na
bima ya gari na usajili faini ni Sh 15,000 hadi Sh 50,000 au kifungo cha miaka
mitano jela.
Dereva kutofunga mkanda faini ni Sh 15,000
au jela miezi sita, abiria aliyekaa mbele bila kufunga mkanda faini ni Sh 30,000
au jela miezi sita au vyote huku abiria wa nyuma asiyefunga mkanda sheria iko
kimya.
Ilieleza kuwa gari ikibainika kuwa na
kasoro, faini yake ni Sh 30,000 au jela miezi sita au vyote, kutokuwa na kibao
cha pembe tatu faini ni Sh 30,000 hadi Sh 50,000 au jela miezi sita au vyote, kutokuwa
na kasha la huduma ya kwanza, faini ni
Sh 30,000 hadi Sh 50,000 au jela miezi sita au vyote.
Aidha, ilibainisha kuwa kukosa kifaa cha
kuzimia moto faini ni Sh 30,000 hadi Sh 50,000 au kwenda jela miezi sita au
vyote, kutumia simu ya mkononi na kuendesha gari faini ni kati ya Sh 15,000 na Sh
50,000 na kifungo cha kati ya miaka miwili hadi mitano.
Hata hivyo suala la kizimamoto limekuwa
na utata, kwani mmiliki wa gari anapokwenda Mamlaka ya Mapato (TRA) kulipia
leseni ya barabarani, hulazimika kuongeza Sh 30,000 ambazo zinaonesha ni kwa
ajili ya kifaa hicho.
Lakini hata baada ya malipo, mmiliki wa
gari hutakiwa tena kwenda Idara ya Zimamoto na Uokoaji, kukinunua kwa bei hiyo
hiyo ambayo alishailipia TRA na hivyo malipo kufanyika marambili na kuonekana
ni dhuluma pia.
Kwa kosa la kuuzuia askari wa usalama
barabarani kufanya shughuli zao, faini ni
Sh 10,000 hadi Sh 20,000 au jela miezi 12 au kutozidi miaka mitano.
Kwa wanaoendesha pikipiki bila kofia
ngumu faini ni Sh 15,000 hadi Sh 30,000 au jela miezi sita au vyote, lakini
sheria ikiwa haisemi lolote kwa abiria asiyevaa kofia hiyo.
Kujaribu kupita gari la mbele sehemu
isiyoruhusiwa faini ni Sh 10,000 au jela miezi sita au vyote na kupita gari
kushoto faini ni Sh 20,000 au jela miezi sita au vyote.
0 comments:
Post a Comment