Celina Mathew
Zitto Kabwe |
MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe,
amesema tangu mwaka 2008 amewasilisha mara kadhaa bungeni Muswada binafsi wa
kutaka sheria ya maadili kwa viongozi wa umma irekebishwe, licha ya kuwa suala
hilo hadi sasa halijafanyiwa kazi.
Zitto alitoa kauli hiyo jana kumjibu
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ambaye takribani siku nne
zilizopita alimtaka Mbunge huyo wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) kutoanika
mshahara wake peke yake, bali apiganie kubadilishwa kwa sheria hiyo ya maadili
kwa kuwa iliyopo haibani viongozi wanaoficha mali zao nje ya nchi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Zitto
alisema hadi sasa ni takribani miaka minane anawasilisha hoja binafsi kuhusu
kurekebishwa kwa sheria hiyo bungeni, lakini hadi sasa bado haijafanyiwa kazi.
"Hivi ninavyoongea nawe kuna Muswada
wangu bungeni wa mwaka 2008 na Desemba mwaka juzi nikiwa Kigoma Kaskazini hadi
nahamia Kigoma Mjini na jambo hilo nimekuwa nikilifanya mara kwa mara na hadi
sasa naendelea kulipigania," alisema Zitto.
Alipozungumza na gazeti hili mwishoni
mwa wiki, Lissu alimshukia Zitto akimtaka
baada ya kuweka kiwango cha mshahara na mali anazomiliki, apiganie kubadilishwa
kwa sheria ya maadili kwa viongozi wa umma.
Kauli ya Lissu ilikuja siku moja baada
ya Mbunge huyo wa Kigoma Mjini, kuweka hadharani kiwango cha mshahara wake kwa
mwaka kuwa ni zaidi ya Sh milioni 123 pamoja na mali anazomiliki.
Lissu alisema hatua hiyo itawezesha
kubanwa kwa viongozi wenye tabia ya kuficha mali zao nje ya nchi kuacha, kwa
kuwa iliyopo sasa haina meno.
Alisema kama Zitto anataka viongozi wengine
wafuate nyayo zake ni vema apendekeze sheria hiyo ibadilishwe, kwa kuwa iliyopo
inaelekeza idadi ya mali ipelekwe kwa Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma
jambo ambalo si zuri.
"Kama Zitto anataka kuwepo uwazi
kwa mali za viongozi, alipaswa kupigania kwanza sheria ili Kamishna asiishie
kupokea taarifa bali aitangaze hadharani ili umma utambue na mfumo huo ubane
kila mtu," alisema.
Alisema haina maana kuonesha mtu yuko tofauti
na wengine, wakati sheria iliyopo haina maana yoyote na haimbani mtu kueleza
mali alizonazo wala kuweka zote hadharani.
0 comments:
Post a Comment