Kauli ya Dk Magufuli Kagera yachambuliwa


*Ni ya waathirika kujenga nyumba, kulima chakula
*Aungwa mkono kwa kuwa mkweli, wengine wanuna

Waandishi Wetu

KAULI ya Rais John Magufuli kuhusu Serikali kutojengea waathirika wa tetemeko mkoani Kagera imepokewa kwa hisia tofauti, upande mmoja ukimuunga mkono na kumpongeza huku mwingine ukimpinga.

Upandwe unaounga mkono umesema aliyosema Rais ni uhalisia na ameendelea kusimamia ukweli na kuacha kudanganya wananchi na kuwajengea matumaini hewa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana amesema licha ya watu wengi kuipokea hotuba ya Rais Magufuli kwa mtazamo hasi, lakini ni dhahiri ameendelea kuonesha jinsi alivyo mkweli katika kila jambo ambalo Serikali yake inafanya na kumfanya azidi kukubalika kwa wananchi.

“Ukweli wa Rais umekuwa ukimsaidia sana hasa pale anapofanya jambo ambalo wapinzani wanalichukulia kwa mtazamo hasi, na ndiyo maana hata ukisikiliza hotuba yake jana (juzi) utaona wananchi walikuwa wakimshangilia kutokana na kusema ukweli huku akiwasisitiza wafanye kazi,” alisema Bana.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk Richard Mbunda naye aliunga mkono kauli ya Rais ya kwamba wapo walioamua kuvunja nyumba zao waliposikia kwamba Serikali itajenga upya nyumba zote zilizoathiriwa huku akisema kitendo cha Rais kuwaambia watu wasitarajie kuletewa chakula cha msaada kitawahamasisha kufanya kazi zaidi.

Mbunda alisema kitendo cha Serikali pia kuichukua sekondari ya Omumwani ni cha manufaa, kwani kinazidisha idadi ya shule ambazo zitawezesha watoto wengi masikini kusoma zaidi kwani hivi sasa elimu ni bure.

“Huwezi kujenga nyumba ya kila mtu ambaye ameathirika, watu wanaweza kuchukua suala la Bukoba kisiasa, lakini tunapaswa kujiuliza hivi fedha zilizochangwa zingeweza kuhudumia idadi ya kaya 2,000 zilizokumbwa na tetemeko?

“Nafikiri Rais amefanya busara kuongea ukweli, kuliko angeahidi kuwajengea nyumba waathirika halafu baadaye Serikali ishindwe kutimiza ahadi hiyo kwa kukosa fedha,” alisema Mbunda.

Wanaopinga

Kwa upande wa waliopinga kauli na msimamo wa Rais Magufuli, walisema hotuba hiyo ililenga kuonesha jinsi Rais asivyoguswa na tukio hilo.

Walisema kauli kama hiyo kwa waathirika kutojengewa nyumba huku wakiwa wanajua fedha zilichangwa kwa ajili yao, ni kinyume na haki za binadamu.

“Rais alipaswa kuonesha jinsi alivyoguswa na maafa yale, lakini kuwaambia wananchi wafanye kazi bila mpango wa kuwajengea nyumba  kiliwanyong’onyeza kwani kila mmoja anatambua kuwa watu waliwachangia na si Serikali,” alisema Mkurugenzi wa LHRC, Hellen Kijo-Bisimba.

Mkurugenzi huyo aliongeza: “Kusema kwamba hakuna serikali inayojenga nyumba za waathirika ni uongo, kwani hivi karibuni Waziri Mkuu wa Italia, Paolo Gentilon aliahidi kuwajengea wananchi waliothirika na maafa na si hapo tu, tumeshuhudia Marekani na Mexico zikiwajengea wananchi wao nyumba zilizoathirika kwa kimbunga.”

Kijo-Bisimba alifananisha kitendo cha Serikali kuchukua fedha za misaada zilizochangwa kusaidia wananchi mmoja mmoja, kuwa ni sawa na kuwadhulumu kwani hata wakisaidiwa na ndugu kama alivyosema Rais, misaada haiwezi kutosha na kusema kiongozi huyo alipaswa kuonesha kuwa ni  Rais wa wanyonge kwa vitendo.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu aliunga mkono kauli ya Kijo-Bisimba akisema hata Italia, Marekani na Mexico zilisaidia kujenga nyumba za waathirika wa tetemeko, kimbunga na maafuriko na kuongeza kwamba kauli ya Rais haikuwa rafiki kwa wananchi kutokana na matatizo waliyopata.

“Serikali ilipaswa kuwa na fungu la miradi si kuchukua fedha za waathirika kujenga majengo ya taasisi zao, ameirudisha serikalini shule ya CCM ya Omumwani baada ya kupiga kelele kuwa fedha za michango zinatumika kujenga miradi ya chama chake,” alisema Baregu.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima (AFP), Rashid Rai alieleza kushangazwa na tamko la Rais kubariki
fedha za michango kupelekwa kwenye miradi ya maendeleo, huku wananchi wakibaki kwenye mazingira magumu, licha ya fedha zilizochangwa kuelezwa ni kwa ajili yao.

“AFP ilichanga mifuko ya saruji 50 na kilo 100 za unga wa dona, hatukuchanga kwa ajili ya Serikali bali wananchi ambao tulihitaji wanufaike na misaada ile, hata akaunti ya benki waliyofungua ilikuwa na jina la Akaunti ya Kuchangia Waathirika. Kama walikuwa wanazihitaji wafanyie miradi yao kwa nini walitumia jina hilo?” Alihoji Rai.

Katibu Mkuu wa NLD, Tozzy Matwanga alisema hotuba ya Rais ilijaa uonevu huku ikiwa inaonesha jinsi Serikali isivyojali matatizo ya wananchi wanapokuwa wamepatwa na maafa, huku akisema kutumia fedha zilizochangwa na taasisi, mashirika na kampuni za ndani na nje kujengea miradi ya Serikali inaweza kusababisha wadau kuacha kuchanga tena yakitokea maafa kama hayo.

“Kauli ya Bukoba inaendana na aliyoitoa kwa wananchi wa Kahama ambao walikumbwa na maafuriko akiwataka kufanya kazi na hawatajengewa nyumba zao ilhali Rais Jakaya Kikwete alikuwa ameahidi kuwajengea,” alisema Matwanga.

Waathirika

Baadhi ya wakazi wa Kagera wamesema kauli ya Rais Magufuli, kwamba hakuna chakula cha Serikali imewashitua na kuwashangaza, wakisema Serikali ina wajibu wa kusaidia wananchi wake.

Wakizungumza na gazeti hili walisema hawakutarajia kiongozi wa nchi kutoa kauli kama hiyo ambayo inawaondolea imani kwamba angewasaidia.

Mkazi wa manispaa ya Bukoba, Sadick Rweyemamu alisema: “Ni kweli Serikali haina shamba, lakini pale wananchi wanapohitaji msaada ina wajibu wa kuwasaidia. Rais kusema hivyo binafsi nilishituka kwa kuwa nilitarajia angetwambia Serikali iko pamoja nasi kwa hali yoyote ile hasa akizingatia matatizo tuliyonayo.”

Abubakari Sadick mfanyabishara wa ndizi katika manispaa hiyo alisema wananchi wanapopata matatizo Serikali iwajibike kuwasaidia na si kutafuta sababu zingine.

“Wananchi wana wajibu wa kulima, lakini unaweza ukalima usipate kitu, sasa hapo litakapokuja baa la njaa wananchi hawa watasaidiwa na nani kama Serikali inasema hivyo? Serikali haiwezi kukwepa kusaidia wananchi wake kwa njia yoyote ile,” alisema Saick.

Emmanuel Kaiza wa Muleba alisema Serikali kusema haina shamba ni kudharau wananchi na  haikupaswa kutoa kauli kama hiyo.

"Rais akisema jambo ni Serikali imesema. Mimi naona kuwa wametudharau wananchi, sijui wanataka tusaidiwe na nani. Nakumbuka Serikali zote zilizopita ikitokea njaa tulikuwa tunasaidiwa, kwani zilikuwa na mashamba?" Alihoji Kaiza.

Kuhusu kujenga nyumba wenyewe Sadick alisema tangu awali Serikali ingewambia kufanya hivyo kungekuwa hakuna tatizo, ila ilikosea kutoa ahadi ambazo haikuzitekeleza ikiwamo ni pamoja na kupewa mabati na saruji.

Juzi akiwa Kagera, Rais Magufuli akizungumza na wakazi wa mkoa huo, alitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo kuwa hakuna chakula na Serikali haina chakula wala shamba kwa sababu mvua imenyesha kila mtu anatakiwa kulima.

‘’Lazima niwaeleze ukweli, kwa kuwa msema ukweli ni mpenzi wa Mungu, mvua zimenyesha watu tufanye kazi, Serikali tusimamie yale mahitaji muhimu kwa Watanzania, tutengeneze reli, tujenge hospitali, tununue dawa, tununue ndege, tulete umeme,’’ alisema Rais Magufuli.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo