Waandishi Wetu
BENKI za CRDB na NMB zimesitisha mikopo kwa
watumishi wa umma na baadhi ya taasisi binafsi, taarifa za uhakika zimeeleza.
Hali hiyo imejitokeza huku Watanzania wengi
wakilalamikia hali ngumu ya kiuchumi, wakati wakikabiliwa na majukumu ya
kijamii na kifamilia hasa kipindi hiki shule zinapofunguliwa.
Taarifa za uhakika kutoka ndani na nje ya benki
hizo, zimeeleza kuwa kusitishwa kwa mikopo hiyo kulianza mwishoni mwa mwaka
jana.
Kwa mujibu wa taarifa hizo watumishi wote wa umma
waliotaka kukopa fedha kutoka CRDB na NMB mwishoni mwa mwaka jana, kwa ajili ya
kufanikisha mambo mbalimbali ikiwamo ada za shule na kodi za nyumba waligonga
mwamba.
Hata hivyo, wasemaji wa benki hizo mara kadhaa
walipotafutwa, hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo huku wakiomba mwandishi
arudi ofisini na kuandika maswali kisha kuyatuma kwao ili yapewe majibu.
Mmoja wa watumishi wa halmashauri kutoka mkoa wa
Tanga, alisema amekuwa akiulizia uwezekano wa kupata mkopo NMB kwa zaidi ya miezi
miwili sasa bila mafanikio.
“NMB walisitisha utoaji mikopo, nimekwenda
kufuatilia kwa zaidi ya miezi miwili hakuna mafanikio, wanasema hawajaanza
kutoa mikopo,” alisema mtumishi huyo.
Mwingine anayefanya kazi kwenye taasisi ya umma Dar
es Salaam, aliliambia gazeti hilo, kwamba hitaji lake la mkopo kutoka NMB
limekwama baada ya kuambiwa imesitishwa.
Mfanyakazi wa moja ya taasisi za Serikali mkoani
Arusha aliyejitaja kwa jina moja na Michael, alisema alifika kwenye moja ya
matawi ya CRDB Novemba mwaka jana na kupewa fomu ya mkopo, lakini alipoirejesha
ili ihakikiwe, akaambiwa mikopo imesitishwa.
Michael alisema alipouliza itarejeshwa lini,
alijibiwa kuwa haijulikani na kwamba watendaji kwenye matawi ya benki hiyo
wanasubiri taarifa kutoka makao makuu.
“Ikiwa tayari kuanza tena kutoa mikopo makao makuu
watatuandikia barua, nasi tutawajulisha na kuanza kukopesha wateja wetu,”
alisema Michael akinukuu majibu ya mtendaji wa tawi la CRDB.
Hata hivyo, taarifa zaidi zinaonesha kuwa CRDB imesitisha
utoaji mikopo hata kwa taasisi na mashirika binafsi.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kwamba kusitishwa
kwa utoaji mikopo kulitokana na sababu mbalimbali likiwamo suala la watumishi
hewa.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, tatizo la watumishi
hewa limeathiri pia utendaji wa benki hizo kutokana na baadhi ya wakopaji
kutoweka na kuacha kulipa madeni yao baada ya uhakiki wa watumishi serikalini,
jambo linalozitia hasara benki.
Hata hivyo, baadhi ya watendaji wa benki hizo
walisema kusitishwa kwa utoaji mikopo, kulitokana na sababu mbalimbali hasa
kupisha uhakiki wa watumishi wa umma.
“Unajua Serikali inafanya uhakiki wa watumishi,
sasa huwezi kuendelea kutoa mikopo kwa watu ambao bado wanahakikiwa,” alisema
mtumishi huyo wa NMB aliyeomba jina lake lisiandikwe kwa kuwa si msemaji.
0 comments:
Post a Comment