Peter Akaro
KUTOFAHAMIANA
vizuri, kuhifadhi vitu nyoyoni na wasiwasi juu ya ndoa baina ya wapenzi,
kumetajwa kuwa sababu ya wapenzi kukimbiana siku ya harusi.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Mtaalamu wa Saikolojia na Uhusiano wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), Dk Chris Mauki alisema watu wengi hufikia kufunga ndoa wakiwa
hawajajuana vizuri.
“Kwa
hiyo jinsi wanavyochukulia siku yao ya harusi, kuna uwezekano mkubwa wa vitu
wasivyovijua kuibuka na kukimbia ndoa,” alisema.
Kauli
ya mtaalamu huyo imekuja baada ya mfululizo wa matukio ya wapenzi kukimbiana
siku ya harusi.
Itakumbukwa
kuwa wiki iliyopita Arusha kuliripotiwa kisa cha binti Sarah Sumaye kutoweka baada
ya kumalizika sherehe ya mwago.
Tukio
kama hilo liliripotiwa Desemba mwaka jana Mbeya ambapo Bwana harusi Samwel Mwakalobo
alitoweka saa chache kabla ya ndoa.
Hata
hivyo, Bwana harusi huyo alijirudi na kufunga ndoa na mchumba wake huyo baada ya
kuomba radhi na kueleza kuwa alichanganyikiwa.
Kutokana
na hali hiyo, Mauki alisema wengi wanaokimbia au kuoana na kesho yake kuachana,
ni kwa sababu mmoja hugundua vitu vinavyomkwaza na wakati huo muda umeshakwenda,
hivyo fursa rahisi ya kulikabili hilo huwa ni kukimbia.
“Lakini
kama wangekuwa na muda mzuri wa kuchunguzana, hivi vitu vingepungua na vitu
vingine huwa ni vya kawaida sana, ila anapokuja kuvigundua ndipo hukimbia au kupigana
vibao siku ya harusi,” alisema.
Alisema
ni vema kwa wapenzi kuwekana wazi kwa mambo mazuri yanayowahusu wao na ndoa
yao, ndugu wanaowazunguka, si kuficha na jambo linakuja kugundulika kwa ghafla,
hapo ni lazima mmoja atakimbia.
“Kwa
mfano siku ya harusi anakuja kugundua kulikuwa na uhusiano ambao haujafa na
mpenzi wake mwingine ... hilo ni tunda la kutofahamiana kwa muda mrefu.
“Wengi
hujiuliza hiki kitu nitakiweza? Kinapomtokea hukumbwa hofu na kwa kuwa hukosa
wa kumweleza huvimeza, kwa sababu ya kuogopa watu watamwangaliaje, hivyo
kujikuta akiingia hivyo hivyo na mwishowe huachana,” alisema Mauki.
Mtaalamu
huyo alisema wapenzi wanaokimbiana na baadaye kuja kuoana tena uwezekano wa
kudumu kwenye ndoa huwa ni mdogo kwa sababu huingia wakiwa tayari na matatizo.
“Ndivyo
inavyoonesha, matatizo walioingia nayo hayafukiwi na hayafi, ni moto unaofukiwa
na baadaye kuwaka.
“Wengi
wanakuja kuachana na ukiwauliza tatizo lilianza lini, watakwambia lilianza muda
mrefu,” alisema Mauki.
Ili
jamii kuepuka matukio kama hayo alishauri wapenzi kuchunguzana kwa muda wa
kutosha, wazazi wasishinikize watoto kuingia kwenye ndoa na kusisitiza
kufahamiana na ndugu wa pande zote mbili.
“Muda
wa kufahamiana usiwe mrefu wala mfupi sana, uhusiano wowote unaokuta labda
wamefahamiana kwa mwaka mmoja una matatizo, kuna uwezekana mdogo wa kudumu,”
alisema Mauki.
0 comments:
Post a Comment