Grace Gurisha
RAIA wa China, Yang Feng Glan ‘Malkia wa Meno ya Tembo’ anayetuhumiwa
kusafirisha meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni 5.4 anaendelea kubaki
rumande baada ya kesi yake kuahirishwa kutokana na hakimu kuwa likizo.
Kesi hiyo iliahirishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi,
Victoria Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa sababu Hakimu Mkazi Huruma Shahidi
anayesikiliza kesi hiyo yuko likizo, kwa hiyo ikalazimika kuahirishwa, ambapo
mshitakiwa alitakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Januari 16, Glan na wenzake wanatarajiwa kusomewa maelezo
hayo. Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama hiyo, baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka
(DPP), Biswalo Mganga kuwasilisha hati ya kuruhusu kusikilizwa kesi hiyo, kwa
sababu kisheria inasikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es
Salaam.
Awali, Wakili Faraja Nchimbi alidai kuwa Glan na wenzake,
Salvius Matembo na Manase Philemon walikutwa wakisafirisha meno hayo ya tembo
vipande 706, vyenye uzito wa kilo 11,889 bila kibali cha Mkurugenzi wa
Wanyamapori.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari mosi, 2000
na Mei 22, 2014, ambapo kwa mara ya kwanza walipandishwa kizimbani Oktoba 7
mwaka jana. Washitakiwa hao pia wanakabiliwa na mashitaka mengine ya
kujihusisha na uhalifu wa kupanga, kukusanya, kusafirisha na kuuza meno hayo
bila kibali cha Mkurugenzi huyo.
Mbali na kesi hiyo, mshitakiwa Philemano anakabiliwa na mashitaka
mengine ya kutoroka akiwa chini ya ulinzi wa Polisi ambapo ilidaiwa kuwa Mei 21, 2014, akiwa Sinza
Palestina, Kinondoni, alitoroka polisi alipokamatwa na nyara hizo za Serikali.
0 comments:
Post a Comment