Salha Mohamed
Kassim Majaliwa |
SERIKALI imefuta posho za vitafunwa katika
halmashauri na kuelekeza fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo.
Posho hizo ni kwenye halmashauri zote
nchini ambazo hazipo kwa mujibu wa sheria, huku ikitoa siku tatu kwa watumishi wa
Halmashauri ya Kigamboni ambao hawajaripoti kazini kujieleza.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea miradi iliyopo kwenye Halmashauri ya
Kigamboni.
Majaliwa alisema Serikali ina taarifa ya
kuwa katika wilaya ya Ilala, wamekuwa wakitumia zaidi ya Sh milioni 400 za
posho ambazo hazikuwa kwenye utaratibu.
“Wilaya ya Ilala walikuwa wakitumia Sh
milioni 400 huku Temeke wakitumia Sh milioni 186, Kinondoni Sh bilioni
mbili.
“Hivyo vitafunwa kwa lugha nyingine bites,
lakini pia Ubungo wanatumia Sh milioni 960 huku Kigamboni ikiwa ni Sh milioni
54 sasa tumefuta posho hizo kuanzia leo (jana),” alisema.
Aliongeza kuwa wakurugenzi wanapaswa
kuhakikisha fedha hizo hazitolewi, huku akibainisha kuwa atakayebainika kukiuka
agizo hilo atafukuzwa kazi.
Alisema Serikali haitampa mtu fedha za
maendeleo mkononi bali zitawekwa kwenye akaunti za halmashauri.
Aliongeza kuwa anafahamu awali madiwani
walikuwa wakipewa fedha za maendeleo mkononi, lakini sasa zitawekwa kwenye
akaunti za halmashauri
Akizungumzia hatua ya watumishi 10 wa Halmashauri
hiyo ambao hawakufika ofisini, Majaliwa alisema: "Nimeambiwa kuwa
watumishi 1,626 wameripoti kwenye vituo vyao vya kazi kwenye Halmashauri hii
mpya ya Kigamboni lakini wapo hao 10 ambao bado.
“Sasa natoa maagizo kuwa nimewapa siku
tatu tu kuanzia leo (jana) wahakikishe wanaripoti, wasipofanya hivyo tutawafuta
kazi," alisema.
Aliwataka watumishi wa Serikali kufanya
kazi ili kuendana na kasi ya Rais John Magufuli
kwa kwenda kusikiliza matatizo ya wananchi.
“Ni lazima watumishi kuhakikisha
wanaweka utaratibu wa kutembelea wananchi waliko na kusikiliza kero zao, mtumishi
anawajibika kwa umma, hivyo ni muhimu kuwafuata wananchi na kuwasikiliza,
lakini mnapotekeleza majukumu yenu hakikisheni mnawahudumia vizuri na kwa staha,"
alisema.
0 comments:
Post a Comment