Badrudin Yahaya
Anna Mghwira |
MWENYEKITI wa Chama cha ACT - Wazelendo,
Anna Mghwira, amewashauri wataalamu wa masuala ya kilimo nchini kuwapa njia bora
wakulima ili wapate mazao ya kutosha badala ya kuwashawishi watumie mbegu za
kisasa pekee.
Mghwira amesema mbegu nyingi za kisasa
zinazotengenezwa viwandani na kuuzwa kwa ajili ya shughuli za kilimo hazina
ubora hata wa kuishi katika misimu miwili ya kilimo, hivyo kuwafanya wakulima
kulazimika kununua mbegu kila msimu wa kilimo unapofika.
Alisema hayo katika mdahalo maalumu wa
kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa na runinga ya Azam Two alipokuwa na
Mratibu wa Mtandao wa Baionaia, Abdallah Ramadhan.
Walikuwa wanazungumzia tatizo la njaa
ambalo limeanza kutokea katika baadhi ya maeneo ya nchi na kuanza kutishia
amani.
“Kinachotatiza nchini kwasasa hadi
kufikia hatua ya kuelekea katika baa la njaa ni kwamba wataalamu wamekuwa
wakilazimisha wakulima watumie mbegu za viwandani, lakini mbegu hizo hazina
ubora ambao unatakiwa na hivyo ni vyema tukatumia mbegu za asili tu,” alisema.
Kwa mujibu wa mgombea huyo wa urais wa
mwaka 2015, wataalamu wanatakiwa kufanya tafiti za kutosha na kuwapatia
ufumbuzi wakulima wa kuhusu namna ya kulima kwa kutumia mbegu asili bila kupata
matatizo.
Aliwanyooshea kidole wananchi kuhusu
hali ya mabadiliko ya tabia ya nchi akisema wanahusika kwa asilimia kubwa wa kulipelekea
Taifa katika hali ya kuwa jangwa kutokana na ukosefu wa mvua kwa muda mwafaka.
Alishauri wananchi kutafuta namna
nyingine ya nishati na si kuendelea kukataa miti kwaajili ya kuchomea mkaa kitu
ambacho kinapelekea kuteketeza misitu.
Kwa upande wake, Ramadhan alisema kuwa
matumizi ya mbegu za kisasa yana faida kubwa ikiwamo usalama, kwani kuna mbegu
za aina nyingi zikiwemo zile za kustahamili ukame ambao au ukosefu wa mvua kwa
kipindi kirefu kama ilivyo hivi sasa nchini.
Mratibu huyo pia alisema katika hali ya
kukabiliana na njaa wakulima wanatakiwa kubadili mawazo yao ya kuzalisha mazao
ya aina moja na hivyo waanze kujenga tabia ya kuwa wanachanganya mazao ya aina
tofauti ili hata ikitokea madhara basi wasikose kabisa hata chakula kidogo.
“Ili kukabiliana na hali ya njaa ambayo
inalikabili taifa kwasasa basi ni vyema wakulima wetu wakaweka tabia ya
kuchanganya mazao tofauti shambani ili wasije wakakosa kitu cha kuvuna,”
alisema.
Alisema kuwa mbali na aina hiyo ya
kilimo kuwa itasaidia katika kuwapatia mazao wananchi lakini pia njia hiyo
inasaidia kutunza ardhi.
0 comments:
Post a Comment