UTT yatakiwa kukopesha wakulima


Mwandishi Wetu


Dk Ashatu Kijaji
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji, ameitaka Taasisi ya Utoaji Mikopo na Huduma za Kifedha ya 'UTT Microfinance' kuandaa mpango mkakati wa kufikia wakulima vijijini na kuwapa mikopo itakayowasaidia kuzalisha mazao kwa wingi.

Akizungumza jana kwenye hafla ya kuzindua Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi hiyo, Dk Kijaji alisema Tanzania ya Viwanda inayotajwa, pia itategemea wakulima kufikia malengo hayo.

"Naipongeza sana UTT kwa utendaji wake wa kazi na hasa kwa Bodi iliyomaliza muda wake, kwa Bodi mpya ninayoizindua leo, iangalie namna ya kufikia wakulima vijijini na kuwapa mikopo nafuu ili kuboresha uzalishaji wao," alisema Kijaji.

Alisema viwanda vitakavyoanzishwa nchini vingi vitategemea malighafi kutoka ndani ya nchi yakiwemo mazao ya wananchi vijijini.

"Serikali inataka kuona taasisi zake zote za kifedha zilizoanzishwa zikitoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wananchi, hii itasaidia kuboresha maisha kwa mwananchi mmoja mmoja," alifafanua.

Alisema pamoja na mafanikio waliyopata UTT kwa miaka mitatu, taasisi hiyo inapaswa sasa ijipange kutoa elimu kwa wajasiriamali na kuwaibua.

Awali, akimkaribisha Naibu Waziri, Ofisa Mtendaji Mkuu wa UTT, James Washima alisema Serikali haikufanya makosa kuanzisha taasisi hiyo, kwa kuwa katika miaka miatatu tangu kuanzishwa kwake, imefikia zaidi ya wajasiriamali 23,513 huku Sh bilioni 29.13 zilitolewa mikopo kwa wananchi hao.

Alisema katika kipindi hicho, matawi 12 yalifunguliwa katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Zanzibar na Dar es Salaam.

Bodi iliyozinduliwa na Naibu Waziri Kijaji, yenye wajumbe wanne inaongozwa na Mwenyekiti, Godwin Mjema, na itakuwa madarakani kwa miaka mitatu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo