Grace Gurisha
HATIMAYE raia wa China, Fu Chang Feng (50), na wenzake
wanaotuhumiwa kwa kukutwa na nyavu haramu za kuvulia samaki zenye thamani ya Sh
bilioni 7.4 wamepata dhamana, baada ya kuwasilisha hati za mali zisizohamishika
zenye thamani ya nusu ya fedha hizo.
Washitakiwa wengine waliopata dhamana jana ni Jeremah
Kepenge (40) na raia wa India, Ally Raza (34), ambapo wengine walipeleka maombi
ya dhamana Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama Kuu
Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi yaani Mahakama ya Ufisadi.
Walifanya hivyo kutokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, Dar es Salaam kisheria kukosa mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, kwa
hiyo mahakama hizo zilitoa masharti ya dhamana ambapo Mahakama ya Kisutu
ilithibitisha masharti hayo na kuwaacha kwa dhamana.
Kepenge aliachwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya
kuwa na hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh bilioni 4.4 huku Raza
akiachwa baada ya kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh
bilioni 2.5.
Pia washitakiwa walitakiwa kuwa na wadhamini wawili kila
mmoja ambao ni watumishi wa umma na wasitoke nje ya Dar es Salaam bila kibali
kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, kukabidhi hati zao za
kusafiria na kuripoti mara moja kwa wiki katika kituo cha Polisi cha Bandari.
Katika mashitaka ya kwanza, ilidaiwa kuwa Oktoba 4 mwaka jana,
Feng akiwa Kurasini Shimo la Udongo, Temeke, aliingiza nchini kontena namba
TCNU 9551 946 kutoka Shangai, China, likiwa na mabegi 499 ya nyavu aina monofilament
zenye thamani ya Sh bilioni 7.4.
Katika mashitaka la pili, dhidi ya washitakiwa wote,
Oktoba 5, wakiwa Ilala barabara ya Mafuriko, walikutwa wakimiliki na kuhifadhi
mabegi 325 yenye vipande 187 vya nyavu hizo zenye thamani ya Sh bilioni 15.1
zikitumika nchini.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo hiyo eneo hilo hilo, washitakiwa
walikutwa wamehifadhi mabegi 50 yeye vipande vya nyavu za kuvulia samaki aina
ya gillnet zenye ukubwa wa inchi zisizopungua tatu zenye thamani ya Sh milioni
300.
0 comments:
Post a Comment