Sharifa Marira
David Kafulila |
WAKATI Sakata la ‘kutumbuliwa’ kwa
aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Felchesmi Mramba, likiendelea
kufukuta, aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ameishauri Serikali
kutafuta njia za kulikomboa shirika hilo ili liimarike badala ya kuendelea
kulipa fedha ambayo ingeweza kutumika kwa mambo mengine.
Kafulila amesema hadi sasa Tanesco
inabebwa na Serikali kiasi kwamba kila mwaka zaidi ya Sh bilioni 400 kutoka Hazina
zinakwenda kuibeba wakati ruzuku ya mbolea mwaka jana ilikuwa Sh milioni 78 na
mwaka huu Sh bilioni 10.
Akizungumza na JAMBOLEO jana, Kafulila
alisema “unaweza kuona wananchi ambao asilimia 70 wanategemea kilimo,
wanasahauliwa ili kuibeba Tanesco maradufu. Tanesco inatumia sehemu ndogo ya
mapato yake kufanya ukarabati ambayo haizidi asilimia nane, wakati inatakiwa
asilimia 15 ya mapato yake ielekezwe kwenye ukarabati wa miundombinu yao ili kupunguza
umeme unaopotea''
Alisema Tanesco inanunua umeme
unapoingia kwenye gridi ya taifa lakini inauza wakati unatoka kwenye gridi hiyo
kuingia kwa mteja ambapo njiani karibu asilimia 30 inakuwa imepotea.
Kafulila alisema madeni ya Tanesco
yanatokana na mikataba mibovu hususan malipo ya tozo za uwekezaji, miundombinu
chakavu kwa maana ya gridi inayosababisha umeme kupotea kwa karibu asilimia 30
ya unaozalishwa.
“Tanesco haina namna ya kukabili hilo
deni, kwani ni mikono ya wakubwa ndiyo iliyosababisha mikataba hiyo na namna
pekee ni Serikali kutaifisha mitambo ya IPTL ili kuipunguzia mzigo Tanesco,
kwani inalipwa karibu Sh bilioni saba kwa mwezi wakati vigezo vyote hawastahili,”
alisema Kafulila na kuongeza:
“Kama Serikali inaogopa IPTL basi ibebe
deni la Tanesco ambalo Desemba mwaka jana lilifika karibu Sh bilioni 700,
zinalipwa kwa kodi za wananchi, kwani Serikali itakuwa imekosa ubavu wa
kuitumbua IPTL na hasara yake ndiyo tunabeba wananchi wa kawaida,” alisema.
0 comments:
Post a Comment