Moses Ng’wat, Mbeya
MFANYABIASHARA
ndogondogo ‘mmachinga’, Jonas John (29), mkazi wa Mbalizi, Mbeya Vijijini,
anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kufukua kaburi la mtu mwenye ualbino, huku
wenzake wawili wakiendelea kutafutwa baada ya kukimbia.
John na wenzake
hao ambao walikimbia, wanadaiwa kufukua kaburi hilo la Mtawa Ofisala
Timayile, aliyefariki dunia mwaka 2010 kwa kuugua na kuzikwa kwenye makaburi ya
kijiji.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari alisema jana kuwa tukio hilo
lilitokea juzi, saa saba usiku, kwenye makaburi ya kitongoji cha Songambele,
kijiji cha Mumba, Mbeya Vijijini.
Akifafanua
kuhusu tukio hilo, Kamanda Kidavashari alisema mtuhumiwa akiwa na wenzake hao walifukua
kaburi hilo kwa lengo la kuchukua baadhi ya viungo vya marehemu.
“Katika
mahojiano ya awali, mtuhumiwa amekiri kufukua kaburi hilo kwa lengo la kuchukua
viungo ili kutumika kwenye mambo yao ya biashara na kuwataja wenzake waliokimbia
na tunaendelea kuwatafuta,” alisema Kidavashari.
Alisema
mtuhumiwa alikamatwa baada ya Polisi kupokea taarifa za siri kutoka kwa raia
wema, ambapo kwa pamoja waliendelea kufuatilia nyendo za mtuhumiwa na wenzake
hadi siku ya tukio walipokutwa wakifukua kaburi hilo.
“Mtuhumiwa
alikutwa ndani ya kaburi akiendelea kufukua na walishafikia sehemu yalipokuwa
mabaki ya mwili wa marehemu,” alisema Kamanda na kuongeza kuwa, wakati akiwa kaburini,
wenzake waliokuwa nje walipoona kundi la watu, walitimua mbio, huku John
akishindwa kutoka na kukamatwa.
Mwenyekiti wa Kitongoji
cha Songambele, Nashon Isega akizungumzia tukio hilo kwa simu alisema John alikamatwa
baada ya wanakijiji kubaini kuwa yeye na wenzake si watu salama.
Alisema mara
kadhaa, watu hao walifika kijijini hapo kutengeneza mazingira ya kufanikisha kufukua
kaburi hilo na ndipo walipowafuatilia hadi kumkamata juzi.
Tukio la
kujaribu kufukua kaburi hilo limeibua hisia zilizoanza kutoweka baada ya miaka
kadhaa kupita tangu matukio ya uchunaji ngozi kutokea mkoani hapa.
0 comments:
Post a Comment